Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
NI MAAJABU BEI ZA NAFAKA ZASHUKA WATEJA WAPUNGUA SOKO LA SEMTEMA SABABU YATAJWA

NI MAAJABU BEI ZA NAFAKA ZASHUKA WATEJA WAPUNGUA SOKO LA SEMTEMA SABABU YATAJWA

Na Angel Magesa (UoI), Matukio Daima Media, Iringa

HAKIKA Maajabu ni mengi na kila uchwao na maajabu yake kama hivyo ndivyo Matukio Daima Media imefunga safari na kukutana na wafanyabiashara  wa nafaka Soko la Semtema, Manispaa ya Iringa, ambao wamedai kuwa biashara ya nafaka imeendelea kudorora licha ya bei za baadhi ya bidhaa, hususan mchele, kushuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miezi iliyopita.

Wafanyabiashara hao wanaojihusisha na uuzaji wa nafaka mbalimbali zikiwemo mchele, mahindi, maharage na njegere, walisema kupungua kwa wateja kumesababisha mzunguko wa fedha kuwa mdogo na kuathiri biashara zao.

Walisema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo wananchi wengi kuwa wamevuna mazao na hivyo kuwa na akiba ya chakula majumbani, jambo linalopunguza mahitaji ya kununua nafaka sokoni.

Sababu nyingine iliyotajwa ni wanafunzi wa vyuo, hususan Chuo Kikuu cha Tumaini, kuwa likizo, hali ambayo imepunguza idadi ya wateja waliokuwa wakitegemewa na wafanyabiashara wa Soko la Semtema.

Mfanyabiashara wa nafaka kwa jumla na rejareja katika soko hilo, Fredrick Dege, amesema bei za nafaka zimepungua kwa kiasi kikubwa, huku mchele ukitajwa kuwa miongoni mwa bidhaa zilizoshuka zaidi.

Alisema awali baadhi ya aina za mchele zilikuwa zikiuzwa hadi Shilingi 3,500 kwa kilo, lakini kwa sasa bei imeshuka hadi kufikia takribani Shilingi 2,000 kwa kilo.

“Kwa sasa bei ya nafaka imeshuka, hasa katika bei ya mchele. 

Japo mauzo yako chini kwa sababu wengi wamevuna na wana vyakula vya kutosha,” alisema Dege.


Kwa upande wake, mfanyabiashara wa nafaka katika Soko hilo, Neema Mushi, alisema licha ya bei kushuka, bado wafanyabiashara wanakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa wateja wa kutosha.

Alisema sehemu kubwa ya wateja wao ni wanafunzi wa vyuo ambao hununua nafaka kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku, hivyo kufungwa kwa vyuo kwa ajili ya likizo kumeathiri moja kwa moja biashara.

“Mzunguko wa biashara umekuwa mdogo. Wanafunzi hawapo, wapo likizo, lakini bei za bidhaa zipo chini,” amesema Neema.

Hata hivyo, kushuka kwa bei hizo kumeelezwa kuwa ni nafuu kwa upande wa watumiaji, ambao sasa wanaweza kununua baadhi ya nafaka kwa gharama ndogo ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

Mkazi wa Iringa na mteja wa nafaka katika Soko la Semtema, Melickzedeck Mboya, amesema kupungua kwa bei kumesaidia kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.

“Kwa sasa maisha yanaenda kwa utofauti. 

Awali bei za mchele zilikuwa juu sana na hali ya uchumi haikuwa vizuri, lakini kwa sasa bei imepungua,” amesema Mboya.

Wafanyabiashara hao walisema wana matumaini kuwa biashara itaimarika baada ya wanafunzi kurejea vyuoni, kutokana na kuwa kundi hilo ni miongoni mwa wateja wakubwa wa nafaka katika soko hilo.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3