NeST YAFUNGUA FURSA ZA ZABUNI ZA SH40.4 TRILIONI KWA WAZAWA
Aug 20, 2026
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
MFUMO wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), umewezesha kutolewa kwa zabuni 397,395 zenye thamani ya Sh40.4 trilioni, huku ukiongeza uwazi, ufanisi na ushiriki wa Watanzania katika fursa za ununuzi wa umma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, ameyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo, Dodoma.
Simba amesema tangu kuanza kutumika kwa NeST, kiwango cha uzingatiaji wa sheria katika michakato ya ununuzi wa umma kimeongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26.
Amesema matumizi ya mfumo huo yamewezesha pia kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Sh27.64 bilioni.
Kwa mujibu wa Simba amesema, NeST imewaondolea wazabuni ulazima wa kusafiri kwenda kuwasilisha nyaraka za zabuni katika taasisi nunuzi, hivyo kupunguza gharama na muda wa kushiriki katika michakato ya ununuzi wa umma.
Amesema kwa sasa mzabuni anaweza kuomba zabuni akiwa mahali popote alipo, jambo ambalo limepanua wigo wa ushiriki kuanzia ngazi za juu hadi Serikali za Mitaa.
“Kwa sasa hata mafundi wa kawaida wanaweza kuomba na kupata kazi ya kushiriki ujenzi katika miradi ya Serikali,” amesema Simba.
Ameongeza kuwa mfumo huo umewezesha utoaji wa zabuni kwa uwazi na usawa katika ngazi za msingi, ikiwamo shule, vituo vya afya na ofisi za kata.
Aidha, amesema utafiti uliofanyika umeonesha kuongezeka kwa ufanisi na uwazi, sambamba na kupungua kwa uzalishaji wa hewa ya ukaa (CO₂e) kwa tani 64,768 katika kipindi cha mwaka 2023/24 hadi 2024/25.
Simba amesema utafiti mwingine unaendelea kuhusu usajili wa NeST katika biashara ya kaboni, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuchangia zaidi ya Sh20 bilioni kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.
Mfumo huo umewezesha pia utekelezaji wa upendeleo wa zabuni na bidhaa za ndani kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.
Simba amesema zabuni zote zenye thamani isiyozidi Sh50 bilioni zimetengwa kwa wazawa pekee, huku wazabuni wa ndani wakipewa upendeleo wa hadi asilimia 10 katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa.
Vilevile, amesema bidhaa za ndani zimepewa upendeleo wa hadi asilimia 15 dhidi ya bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amesema mfumo huo umewezesha utekelezaji wa upendeleo huo kwa njia ya kielektroniki, ambapo wazabuni wa nje hawawezi kuomba zabuni zenye thamani ya chini ya Sh50 bilioni zilizotengwa kwa wazawa.
Katika hatua nyingine, Simba amesema Sheria ya Ununuzi wa Umma imezielekeza taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum, yakiwamo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Amesema hadi sasa makundi maalum 27,946 yamesajiliwa katika NeST, ambapo vijana ni 13,317, wanawake 13,400, wazee 643 na watu wenye ulemavu 586.
Amesema makundi hayo tayari yamepata zabuni zenye jumla ya thamani ya Sh56 bilioni kupitia mfumo huo.
Kwa mujibu wa Simba, PPRA inalenga kufikisha idadi ya makundi maalum yaliyo tayari kuomba zabuni takribani 300,000, kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema mpango huo unalenga kuwapa fursa za ajira na kazi Watanzania ambao hawana uwezo wa kuwa na kampuni, lakini wanaweza kujiunga katika vikundi vya watu watatu au zaidi na kushiriki zabuni za Serikali.
“Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na uchumi jumuishi; kwamba kila Mtanzania ananufaika na anachangia pia kwenye ukuaji wa uchumi,” amesema.
Amesema kundi maalum linaweza kupata zabuni moja yenye thamani ya hadi Sh500 milioni.
Simba amesema suala hilo limepewa nafasi katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, hatua ambayo imeongeza uhamasishaji na usajili wa vikundi.
Aidha, amesema PPRA itashirikiana na Ofisi ya Rais Wizara ya Maendeleo ya Vijana katika kuhamasisha usajili wa vikundi katika Halmashauri zote 184 nchini.
Amewataka Watanzania kujiunga katika vikundi vya watu watatu au zaidi, kuvisajili katika Halmashauri zao na baadaye kusajili vikundi hivyo katika Mfumo wa NeST ili kunufaika na fursa za zabuni za umma.



