MARAIS WA MASHIRIKISHO YA SOKA: INFANTINO ALIVUNJA UAMINIFU
FIFA na rais wake, Gianni Infantino, wametuhumiwa kuvunja uaminifu “kupitia udanganyifu” katika barua ya wazi iliyotolewa na UEFA, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia (AFC).
Barua hiyo, iliyotiwa saini na marais na makatibu wakuu wa mashirikisho hayo, ilisema kuwa mzozo wa hivi karibuni kuhusu pendekezo la Fifa Forward Enterprise (FFE) kimsingi ulihusu “uadilifu wa mchezo, pamoja na uadilifu wa wale waliochaguliwa kuuongoza.”
FFE ingesababisha kuanzishwa kwa kampuni mpya ya kusimamia haki za kibiashara na tiketi za mashindano yote ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia, huku 21% ya kampuni hiyo ikiuzwa kwa kampuni binafsi ya uwekezaji.
Mpango huo ulisitishwa baada ya kukosolewa vikali na mashirikisho kadhaa, yakiongozwa na UEFA, ambayo ilitishia kususia mashindano yote ya FIFA.
“Uaminifu unapovunjwa kupitia udanganyifu, na mtu anapojiona kuwa yuko juu ya jumuiya iliyomkabidhi mamlaka, basi ameachana na wajibu huo,” ilisema barua hiyo.