Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 LINDI: MMUYA ATAKA  VIVUTIO VYA UTALII LINDI NA MTWARA VITANGAZWE ZAIDI KUCHOCHEA UCHUMI WA DIRA 2050

LINDI: MMUYA ATAKA VIVUTIO VYA UTALII LINDI NA MTWARA VITANGAZWE ZAIDI KUCHOCHEA UCHUMI WA DIRA 2050


Na Hadija Omary 

Lindi: Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspa Mmuya, ametoa wito wa kuthamini na kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo nchini kwa kuzigeuza kuwa fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa sekta ya utalii inapaswa kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mmuya ameyasema hayo alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maliasili na Mazingira.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na endelevu unaotumia rasilimali za nchi kwa ufanisi ili kuongeza tija na kuinua ustawi wa wananchi.

"Ili kufikia adhima hiyo, ni lazima tuzithamini rasilimali tulizonazo na kuzibadilisha kuwa fursa za kiuchumi. Sekta ya utalii ina nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo na kuongeza mapato ya taifa," amesema Mmuya.

Ameeleza kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara imebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee vya utalii, lakini bado haijafanikiwa kuvitangaza vya kutosha ili kuvutia watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mmuya, ipo haja ya kuongeza juhudi za kutangaza vivutio hivyo ili viweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa mikoa hiyo na taifa kwa ujumla.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuitangaza sekta ya utalii utasaidia kuongeza idadi ya watalii, kuibua fursa za ajira na biashara, pamoja na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa, amesema wakala huo unaendelea kubaini na kuendeleza maeneo mbalimbali yenye fursa za utalii katika mikoa ya kusini ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi.

Naye Afisa Mhifadhi Mwandamizi wa Mambo ya Kale kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), anayesimamia Hifadhi ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Mency Mbogela, ametoa wito kwa wananchi kutembelea maeneo hayo kujifunza historia na urithi wa taifa pamoja na kufurahia vivutio vya kipekee vilivyopo    


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3