ADEM KUPANUA MAFUNZO YA VIONGOZI WA ELIMU KUINUA UBORA WA ELIMU
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umetangaza kuongeza wigo wa mafunzo kwa viongozi wa sekta ya elimu nchini katika jitihada za kuimarisha uongozi, usimamizi wa shule na kuongeza ubora wa elimu unaotolewa kwa wanafunzi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid Maulid, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo wa kuhakikisha viongozi wa elimu wanapata ujuzi unaowawezesha kukabiliana na mabadiliko ya sekta ya elimu na kusimamia kwa ufanisi taasisi wanazoongoza.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo Agosti 6, 2026 Jijini Dodoma, Dkt. Maulid amesema ADEM imeendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa wakuu wa shule, walimu wakuu, maafisa elimu wa kata, halmashauri na mikoa, wathibiti ubora wa shule pamoja na viongozi wengine wa elimu ili kuongeza uwajibikaji na kuboresha usimamizi wa taasisi za elimu.
Amesema kupitia programu ya Stashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu (DELMA), jumla ya wahitimu 8,599 wamehitimu tangu mwaka 2002 hadi 2025, huku wahitimu 2,263 wakihitimu kupitia programu ya Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) kati ya mwaka 2016 na 2025.
Aidha, amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026, ADEM ilidahili wanafunzi 2,016, wakiwemo 1,634 wa programu ya DELMA na 382 wa DSQA.
Dkt. Maulid amesema mafunzo yanayotolewa yamechangia kuimarika kwa utawala bora katika shule, usimamizi wa rasilimali za elimu, matumizi ya TEHAMA katika uongozi wa shule pamoja na kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa elimu.
Ameongeza kuwa ADEM pia inatekeleza Mradi wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Shule za Awali na Msingi (BOOST), ambapo imepatiwa zaidi ya Shilingi bilioni 16 kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa elimu nchini.
Kupitia mradi huo, zaidi ya walimu wakuu 17,817, waratibu elimu kata zaidi ya 3,900 pamoja na maafisa elimu wa wilaya na mikoa wamepatiwa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu ili kuboresha utoaji wa huduma katika shule za umma.
"Mbali na mafunzo, ADEM imeendelea kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu unaosaidia maboresho ya sera na mifumo ya elimu, huku ikipanua ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na kimataifa ili kuimarisha ubora wa mafunzo na matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu, " Amesema.
Dkt. Maulid amesema kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ADEM inalenga kuongeza udahili wa wanafunzi wa mafunzo ya muda mrefu kutoka 2,016 hadi 3,500, sambamba na kuanzisha programu mpya, kupanua matumizi ya TEHAMA na kuboresha miundombinu ya kampasi zake za Bagamoyo, Mbeya na Mwanza.
Amesema Hatua hizo zinalenga kuzalisha viongozi wa elimu wenye uwezo wa kusimamia mageuzi ya sekta ya elimu na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

.jpeg)
