AJALI YA MABASI YAUA WANANE DODOMA, RC SENYAMULE AFIKA ENEO LA TUKIO NA HOSPITALINI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SIMANZI imetanda mkoani Dodoma baada ya watu wanane kupoteza maisha na wengine 66 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya abiria yaliyokuwa yakitokea pande tofauti za nchi.
Ajali hiyo ilihusisha basi la Isamilo lenye namba za usajili T 428 EXP, lililokuwa likisafiri kutoka Mwanza kuelekea Dar es Salaam, na basi la Libanika Luxury lenye usajili T 897 DUP, lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa watu wanane walifariki dunia katika ajali hiyo, huku majeruhi 66 wakipelekwa kwa haraka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kupata huduma za matibabu.
Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alifika eneo la tukio kufuatilia hali halisi na kujionea hatua zilizokuwa zikichukuliwa na vyombo vya uokoaji na usalama.
Kutoka eneo la ajali, Senyamule alielekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako aliwajulia hali majeruhi na kupokea taarifa kutoka kwa madaktari kuhusu mwenendo wa matibabu yao.
Katika ziara hiyo, alijionea huduma zilizokuwa zikitolewa kwa majeruhi na kuridhishwa na namna timu za afya zilivyojitokeza kuwahudumia, huku akielezwa kuwa majeruhi wamepatiwa matibabu yanayostahili na hali za wengi wao zinaendelea kuimarika.Ajali hiyo imeibua huzuni miongoni mwa wananchi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo chake na mamlaka husika zikiendelea kutoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana.





