WAZIRI DKT GWAJIMA ASIFU MIRADI YA BRAC MAENDELEO MKOA WA IRINGA
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametembelea mkoani Iringa kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania kwa lengo la kutathmini mafanikio, changamoto na mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Gwajima alitembelea baadhi ya miradi inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalum kiuchumi kupitia mafunzo ya ujasiriamali, kilimo, elimu ya stadi za maisha na huduma za maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kama BRAC Maendeleo Tanzania ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa wananchi na kuchochea maendeleo jumuishi nchini.
Alisema juhudi za serikali zimevutia wadau mbalimbali wa maendeleo, akiwemo Black Maendeleo, ambao wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kuwawezesha wanawake kupitia mafunzo, ushauri na miradi ya maendeleo.
“Nawapongeza wanawake kwa hatua mliyoifikia, nawasisitiza kuunda na kuendesha vikundi si jambo rahisi, bali kunahitaji uongozi makini, mshikamano na mafunzo endelevu ili kuhakikisha vikundi vinakuwa imara na vinatimiza malengo yake”
Aidha, alieleza kuwa wanachama wa vikundi wanaweza kufikia hatua ya kujitegemea zaidi kwa kuanzisha biashara binafsi baada ya kupata uzoefu na mtaji kupitia vikundi, huku wakitumia fursa mbalimbali za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha, ikiwemo NMB Bank Plc.
Alibainisha kuwa serikali imeendelea kuweka fedha katika mifuko na programu za uwezeshaji ili wananchi wenye sifa waweze kunufaika kupitia vikundi au kama wajasiriamali binafsi kulingana na hatua ya maendeleo waliyoifikia.
Aidha Dkt Dorothy, alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa elimu na ushauri kwa wanawake ili waweze kutumia vyema fursa walizozipata kupitia Black Maendeleo na kuendeleza safari yao ya kujikwamua kiuchumi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkoa huo Bi Zaina Mlawa alisema kuwa halmashauri itafanya vikao na vikundi hivyo, kusikiliza mipango yao na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha vinaendelea kukua na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, alisisitiza kuwa vikundi vitakavyokidhi vigezo vitawezeshwa kupata mikopo ya halmashauri, akibainisha kuwa tayari kuna vikundi vingine vilivyonufaika na mikopo hiyo baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali na stadi mbalimbali kupitia VETA.
Alieleza kuwa vikundi vilivyowezeshwa hapo awali vimeonyesha mafanikio makubwa katika shughuli zao za kiuchumi, jambo linaloipa halmashauri imani kuwa hata vikundi vipya vitaweza kufanikiwa.
Kwa upande wake, uongozi wa BRAC Maendeleo Tanzania ulieleza kuwa shirika hilo linaendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wanawake, vijana, wakulima na watoto kupitia elimu, uwezeshaji wa kiuchumi, kilimo na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake Meya wa manispaa ya Iringa Ibrahimu Ngwada alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeendelea kutekeleza mpango wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
Alisema kuwa Katika mwaka wa fedha 2025/2026, zaidi ya shilingi milioni 400 zimetolewa kwa makundi hayo, huku baadhi ya wanufaika wakipatiwa vitendea kazi kama pikipiki na bajaji ili kuwasaidia kujiongezea kipato.
Ngwada alisema kuwa mpaka sasa tayari jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zimetolewa kwa programu hiyo katika msimu uliopita
Ziara ya Dkt. Gwajima ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi yenye mchango katika kupunguza umaskini na kuinua ustawi wa jamii nchini.

