Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BALOZI SIRRO AWAKA MRADI WA DARAJA KITANGA KUKWAMA

BALOZI SIRRO AWAKA MRADI WA DARAJA KITANGA KUKWAMA

 


Na Fadhili Abdallah,kigoma

 MWEKEZAJI  kiwanda cha Sukari wilayani Kasulu mkoani Kigoma anadaiwa kukwamisha utekelezaji wa mradi wa daraja la mto Malagarasi kati ya kijiji Kitanga  wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma baada ya daraja hilo kutumiwa na Mwekezaji huyo  kwa shughuli zake za kiwanda wakati taratibu zote za mradi huo kutekelezwa katika kijiji cha Kitanga zikiwa zimekamilika.

 Meneja wa Wakala wa barabara mkoa Kigoma (TANROADS), Mhandisi Elison Mweladzi alitoa maelezo hayo kwa Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro aliyefanya ziara kutembelea na kukagua daraja hilo baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa kijiji cha  Kidagye na Kitanga wilaya ya Kasulu wakieleza kushindwa kukamilika kwa daraja hilo kunakwamisha shughuli zao za uchumi. 

Mhandisi Mweladzi alisema kuwa baada ya kuanza kutekelezwa kwa mradi mkubwa wa barabara ya Manyovu wilaya ya Buhigwe hadi Kabingo wilaya ya Kakonko kwa kiwango cha Lami iliamuliwa kwenye vikao mbalimbali daraja la Chuma lililopo kijiji cha Busungu wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kwenye Mto Malagarasi barabara kuu ya Kigoma hadi Nyakanazi liodnolewe na kupelekwa kwenye kijiji cha Kitanga ili kurahisisha wananchi kuvuka kwa urahisi kutoka Kasulu kuelekea Kibondo.

 Hata hivyo mhandisi huyo alisema kuwa kabla daraja hilo la chuma kufunguliwa Mwekezaji wa kiwanda cha Miwa aliyejenga kiwanda katika kijiji cha Mvugwe wilaya ya Kasulu aliomba daraja hilo lisihamishwe kwani linasaidia shughuli zake za kiwandani katika usafirishaji wa malighafi mbalimbali hivyo mradi huo ukakwamia hapo. 


Kufuatia kauli hiyo Mkuu wa mkoa Kigoma,Balozi Simon Sirro ameitaka TANROADS kuhamisha daraja hilo kutoka kijiji cha Mvugwe na kupelekwa kijiji cha Kidagye wilayani Kasulu kwani mahitaji ya wananchi huko ni makubwa na zipo athari za kiuchumi na kijamii zinazowapata wananchi hao kwa kushindwa kukamilika kwa daraja hilo.

 Balozi Sirro alisema kuwa kutokana na sintofahamu iliyojitokeza na daraja kushindwa kuhamishwa kwa nguvu ya mwekezaji anatarajia kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS na Waziri wa ujenzi kuona daraja hilo linahamishwa na kupeelekwa  katika kijiji cha Kitanga kama  ulivypangwa awali ili  utafutwe utaratibu mwingine wa kusaidia shughuli za uboreshaji wa miundo mbinu katika kiwanda cha Mwekezaji. 

Akizungumza katika mkutano wa hadhara ambao Mkuu wa mkoa Kigoma alifanya na wananchi wa kijiji cha Kigadye diwani wa kata ya Kitanga, Elia Kagoma alisema kuwa kutokuwepo kwa daraja hilo kumedumaza shughuli za kiuchumi za wananchi wa  kijiji hicho kwa kukifanya kuwa kisiwani na kushindwa kupata maendeleo ya haraka.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Kitanga, Thomas Rulila alisema kuwa kutokuwepo kwa daraja kumekuwa na athari kubwa ya kuvusha pikipiki zao kuelekea Kibondo lakini pia imekuwa ikichangia kufanya bei za mazao kuwa chini na wanunuzi kuja kununulia shambani

 Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3