Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI WATAKIWA KUTEMBELEA BANDA LA BODI YA BIMA YA AMANA KUPATA ELIMU

WANANCHI WATAKIWA KUTEMBELEA BANDA LA BODI YA BIMA YA AMANA KUPATA ELIMU

 

Na Matukio DaimaMedia 

Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa 2026 (Sabasaba) ili kupata elimu kuhusu haki zao, majukumu ya taasisi hiyo na namna amana zao zinavyolindwa kisheria.


‎Akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo, Afisa Mwandamizi wa Bodi ya Bima ya Amana, Joyce Shala, amesema taasisi hiyo ya Serikali imepewa jukumu la kulinda amana za wananchi endapo benki au taasisi ya fedha itafungwa au kuwekwa chini ya ufilisi.


"‎Bima ya amana inalenga kuhakikisha wananchi3 wanarejeshewa fedha zao pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake, takribani asilimia 99 ya wateja wa benki hulipwa fidia kwa asilimia 100 ya fedha zao zinazostahili chini ya mfumo huu," amesema Shala.

Amesema kuwa mbali na kulipa fidia, amesema taasisi hiyo pia imepewa jukumu la kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania katika kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwenye benki zenye changamoto za kiuendeshaji, kwa lengo la kulinda mfumo wa fedha na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma za kibenki bila usumbufu.

Aidha, bodi hiyo imewahakikishia Watanzania kuwa fedha wanazoweka katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni zinalindwa kisheria, huku ikitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupata elimu kuhusu huduma zake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

‎‎Katika hatua nyengine, amefafanua kuwa tofauti na bima nyingine, bima ya amana haihitaji mwananchi kuchangia fedha yoyote, kwani kwa mujibu wa sheria benki zote zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ndizo zinazochangia mfuko huo kwa niaba ya wateja wao.

‎Ameongeza kuwa kwa wateja wenye fedha zinazozidi kiwango cha fidia kinachotolewa kisheria, Bodi ya Bima ya Amana huendelea na mchakato wa ufilisi wa benki husika kwa kukusanya mali na madeni ili kuhakikisha wadai wanapatiwa malipo kwa mujibu wa sheria.

‎Shala amesema taasisi hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuwafikia wananchi kupitia maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Huduma za Fedha na programu za elimu katika kanda mbalimbali nchini, ili kuongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa kuweka fedha benki kwa usalama.

‎"Tunataka Watanzania wawe na imani ya kuweka fedha zao benki wakijua kuwa kuna mfumo wa kisheria unaolinda amana zao. Elimu hii tunaitoa bila malipo, hivyo tunakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu na kupata ufafanuzi wa huduma tunazotoa," amesema.

‎Amesema kuwa uwepo wa Bodi ya Bima ya Amana ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha utulivu wa sekta ya fedha na kujenga imani ya wananchi katika mfumo wa benki nchini, kwa lengo la kuhakikisha fedha zao zinalindwa na zinakua salama.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3