WANANCHI WAONYWA KUTUPA TAKA KWENYE MITARO
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI imewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka kwenye mitaro ya maji, ikionya kuwa vitendo hivyo vinaziba mifumo ya maji, husababisha mafuriko na kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Paramagamba Kabudi, amesema usafi wa mazingira ni nguzo muhimu ya afya na maendeleo endelevu, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kulinda mazingira.
Kabudi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo katika kuhakikisha huduma za usafi wa mazingira zinaboreshwa na kuwafikia wananchi wote mijini na vijijini.
"Tunataka Tanzania yenye miji na vijiji safi ni muhimu kuja na mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji wa huduma jumuishi za usafi wa mazingira ili ziwafikie wananchi wote," amesema.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kama sehemu ya kulinda mazingira na afya za wananchi, akibainisha kuwa uongozi wa Rais Samia umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza ajenda ya nishati safi.
Kabudi amesisitiza kuwa uwekezaji katika usafi wa mazingira ni uwekezaji katika afya ya wananchi na akataka kuboreshwa kwa miundombinu ya vyoo katika maeneo ya mikusanyiko pamoja na upatikanaji wa maji ya kunawa mikono ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, ameipongeza EWURA kwa kuandaa kongamano hilo, akisema litasaidia kuibua suluhisho za kudumu za changamoto za usafi wa mazingira.
Amesema vifo vingi vinavyotokana na athari za mazingira husababishwa na shughuli za binadamu, hivyo elimu kwa wananchi inapaswa kupewa kipaumbele ili kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika, hasa kwa watoto.
Naye Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe, amesema kati ya mamlaka 84 za maji nchini, ni 24 pekee zenye mifumo ya kutibu majitaka na tope la kinyesi, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika huduma hizo.
Mahembe amesema kongamano hilo limezindua Mwongozo wa Usimamizi wa Mazingira utakaosaidia kuimarisha usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira nchini, huku EWURA ikiendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za utibuji wa majitaka zinaimarika.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ongezeko la watu mkoani humo linaongeza mahitaji ya huduma za usafi wa mazingira, hivyo yanabaki safi na salama kwa wananchi.










