IRINGA MJINI TUMEPATA MBUNGE WA MFANO ANAYEWASEMEA WANANCHI -MEYA NGWADA
Mbunge wa Iringa mjini Fadhil Ngajilo akifurahi na watu wenye ulemavu wa kusikia baada ya kuwachangia kiasi cha Tsh milioni 1 picha na Matukio Daima Media
Na Matukio Daima Media,
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ya kibunge, akieleza kuwa ameonyesha mfano wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya wananchi wa jimbo lake tofauti na baadhi ya wabunge waliowahi kuliongoza jimbo hilo hapo awali.
Ngwada alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 420 kwa vikundi 28 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hafla iliyofanyika katika Manispaa ya Iringa.
Alisema amekuwa akifuatilia michango ya Mbunge Ngajilo bungeni na kubaini kuwa hoja zake nyingi zimejikita katika kutetea maendeleo ya Jimbo la Iringa Mjini na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi wake.
Alisema pamoja na ukweli kwamba mbunge ni mwakilishi wa wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ana wajibu wa kujadili masuala ya kitaifa, kipaumbele chake kinapaswa kuwa ni kuwasemea wananchi waliomchagua na kuhakikisha mahitaji yao yanapata ufumbuzi kupitia serikali.
Kwa mujibu wa Ngwada, baadhi ya wabunge waliopita walikuwa wakitumia muda mwingi kujadili masuala ya kitaifa bila kuipa uzito wa kutosha agenda ya maendeleo ya Jimbo la Iringa Mjini, hali ambayo kwa sasa imebadilika kutokana na namna Mbunge Ngajilo anavyowasilisha hoja zinazolenga kuboresha huduma na maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
Katika hafla hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ilikabidhi mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 420 kwa vikundi 28 vya ujasiriamali vinavyoundwa na wanufaika 124.
Mikopo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia asilimia ya mapato ya ndani ya halmashauri zinazotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, alisema fedha hizo zinalenga kuongeza mitaji ya wanufaika, kuanzisha biashara mpya na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali ili kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Manispaa.
Mlawa alisema kabla ya kupokea mikopo hiyo, wanufaika walipewa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo ili kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya katika maisha yao na jamii kwa ujumla.
Alieleza kuwa halmashauri itaendelea kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia vikundi vya ujasiriamali, ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza umaskini, kuongeza ajira na kuinua maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Meya Ibrahim Ngwada alisema Halmashauri itaendelea kusimamia kwa karibu matumizi ya mikopo hiyo ili kuhakikisha fedha zinarejeshwa kwa wakati na kufanikisha wananchi wengi zaidi kunufaika na mpango huo.
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na timu ya menejimenti kwa ushirikiano mzuri wanaouonyesha katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi, akisema mafanikio yanayopatikana yanatokana na mshikamano na uwajibikaji wa viongozi na watendaji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na moyo wa kusaidiana, hususan kwa watu wenye mahitaji maalumu, akisisitiza kuwa thamani ya msaada haipimwi kwa ukubwa wake bali kwa dhamira ya kumuinua anayehitaji.
Ngajilo alisema wanufaika wa mikopo wanapaswa kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuwasaidia kuboresha maisha yao na kuongeza kipato cha familia zao. Alionya kuwa matumizi mabaya ya mikopo yamekuwa yakichangia baadhi ya programu za uwezeshaji kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Mbunge huyo pia aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu, akieleza kuwa hatua ya kuruhusu hata mtu mmoja mmoja kunufaika na mikopo badala ya kutegemea vikundi pekee itaongeza fursa kwa wananchi wengi zaidi wanaohitaji mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara zao.
Katika hatua nyingine, Ngajilo alisema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeamua kujenga vibanda vya kisasa katika eneo la Posta kwa ajili ya wafanyabiashara wenye ulemavu, hatua ambayo inalenga kuwapatia mazingira bora ya kufanya biashara na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.
Alisema mpango huo unaunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuhakikisha makundi maalumu yanapata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya taifa.
Mbunge huyo alisisitiza umuhimu wa elimu ya ujasiriamali, akisema pamoja na upatikanaji wa mikopo, wananchi wanahitaji maarifa ya usimamizi wa biashara ili waweze kutumia mitaji yao kwa ufanisi na kuhakikisha biashara zao zinakuwa endelevu.
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kutafuta fursa za kifedha kwa wananchi ambao bado hawajafanikiwa kupata mitaji, ili kuhakikisha kila mwenye nia ya kufanya shughuli za uzalishaji mali anapata nafasi ya kujikwamua kiuchumi.
Ngajilo alisema takwimu zinaonyesha kiwango cha umaskini nchini kinaendelea kupungua katika miaka ya hivi karibuni, akieleza kuwa njia endelevu ya kuendelea kupunguza umaskini ni kuwekeza katika elimu ya ujasiriamali, uwezeshaji wa wananchi pamoja na upatikanaji wa mitaji ya biashara.
Kwa upande wake, mwakilishi wa watu wenye ulemavu, Athumani Hamiss, alimshukuru Mbunge Ngajilo kwa kuwapatia msaada wa usafiri utakaowawezesha kushiriki maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani yatakayofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5.
Alisema msaada huo umeondoa changamoto ya usafiri na kuwapa fursa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo muhimu. TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII
Naye Smani Jili alisema wanathamini mchango huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika juhudi za kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, ushiriki na fursa sawa katika maendeleo ya jamii.

