WANANCHI WATAKIWA KUJIANDAA NA FURSA ZA BWAWA LA KIDUNDA
Jul 24, 2026
Na Matukio Daima Media,Morogoro.
WANANCHI wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mradi wa Bwawa la Kidunda wametakiwa kujiandaa kutumia fursa za kiuchumi zinazotarajiwa kujitokeza baada ya kukamilika kwa mradi huo, ikiwemo kuimarika kwa shughuli za kilimo na ufugaji.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, Nickson Lutenda, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda.
Lutenda amesema Serikali itaendelea kuhakikisha vyanzo vyote vya maji vinavyolisha bwawa hilo vinalindwa ili kuwezesha upatikanaji wa maji wa kudumu na kuhakikisha uwekezaji huo unakuwa endelevu.
Amesema wananchi wanapaswa kuona bwawa hilo siyo tu kama mradi wa maji, bali pia kama chanzo cha fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazoweza kuwanufaisha baada ya kukamilika kwake.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Suffian Ally, amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa bwawa hilo, Sino Hydro Corporation, kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa mvua za El Nino zinazotabiriwa kunyesha mwishoni mwa mwaka 2026.
Ally amesema taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinapaswa kuzingatiwa katika kupanga utekelezaji wa mradi huo ili mvua zisitumike kama sababu ya kusimamisha ujenzi.
Amesema maendeleo ya mradi huo yanaridhisha, hivyo mkandarasi anatakiwa kuweka mikakati ya mapema itakayowezesha kazi kuendelea bila kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Naye Katibu wa Bodi ya Maji ya Taifa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji katika Wizara ya Maji, Robert Sunday, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam na maeneo jirani wanapata huduma ya maji ya uhakika.
Amesema utekelezaji wa mradi huo umewezekana kutokana na uamuzi wa Serikali kutumia fedha za ndani, baada ya wazo la kuujenga kuwepo kwa zaidi ya miaka 50.
Mradi wa Bwawa la Kidunda unagharamiwa kwa fedha za ndani zinazozidi Sh bilioni 300 na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 52.4.
Mwisho



