WAFANYABIASHARA MAWENZI WASITISHA BIASHARA KUPINGA ONGEZEKO LA KODI
Jul 24, 2026
Na Matukio Daima Media,Morogoro
WAFANYABIASHARA wa Soko la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro, wamesitisha shughuli za biashara kwa zaidi ya saa tatu tangu saa 11 alfajiri Juni 24 mwaka huu wakipinga ongezeko la kodi ya meza kutoka Shilingi 10,000 hadi Sh20,000, wakisema hatua hiyo inawaongezea mzigo na kutishia uendelevu wa biashara zao.
Mgomo huo ulianza majira ya saa 11 alfajiri kwa wafanyabiashara kufunga biashara zao hadi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, alipofika sokoni hapo na kuzungumza nao kuhusu malalamiko yao.
Baada ya kusikiliza kero hizo, Kilakala akawataka wafanyabiashara kusitisha kusaini mikataba mipya hadi Jumanne wiki ijayo ili kutoa nafasi ya mazungumzo na kutafuta muafaka kuhusu masuala yanayolalamikiwa.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Farida Juma, amesema ongezeko la kodi limewaathiri kwa kuwa halilingani na hali ya biashara wanazofanya.
"Tunataka suala hili lisikilizwe na mamlaka husika kwa sababu ongezeko hili linatuletea mzigo mkubwa. Tunaomba tupate nafasi ya kukaa pamoja na kujadiliana ili tupate suluhisho," anasema Juma.
Naye Asia Lubamba amesema wafanyabiashara wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu isiyoridhisha, hivyo wanahitaji maboresho kabla ya kuongezewa gharama za uendeshaji wa biashara.
"Kama kodi inaongezeka, tunatarajia pia kuona mazingira ya biashara yakiboreshwa. Hali ya miundombinu ndani ya soko bado ni changamoto kwetu," amesema Lubamba.
Mwenyekiti wa Soko la Mawenzi, Yassin Tonge, amesema wafanyabiashara wanahitaji majadiliano ya pamoja kuhusu mabadiliko ya gharama mbalimbali wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku.
Wafanyabiashara hao pia wamelalamikia gharama ya matumizi ya vyoo kupanda kutoka Sh200 hadi Sh300, pamoja na ushuru unaotozwa katika maeneo mbalimbali kabla ya bidhaa kufikishwa sokoni, wakidai wakati mwingine bidhaa moja inaweza kutozwa ushuru zaidi ya mara moja.
Baada ya kusitisha biashara kwa zaidi ya saa tatu, wafanyabiashara hao wameendelea na shughuli zao baada ya kupewa nafasi ya mazungumzo zaidi na uongozi wa wilaya.
Mwisho


