Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 WANAFUNZI WA UBUNGO WANUFAIKA NA MRADI WA USALAMA BARABARANI

WANAFUNZI WA UBUNGO WANUFAIKA NA MRADI WA USALAMA BARABARANI


Na Matukio DaimaMedia 

Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani limesema mapambano dhidi ya ajali za barabarani hayawezi kufanikiwa kwa nguvu za polisi pekee, likisisitiza ushirikiano wa taasisi za Serikali, sekta binafsi, shule na jamii katika kulinda maisha ya watoto wanaotumia barabara kila siku kwenda na kutoka shuleni.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mradi wa Safe at School, Safe Today and Safer Tomorrow,  ACP Joseph  P. Mwakabonga Operesheni ofisa makao makuu ya salama bararani ( T), amesema watoto ni miongoni mwa watumiaji wa barabara walio katika hatari kubwa ya kupata ajali kutokana na kuongezeka kwa idadi ya vyombo vya usafiri na msongamano wa magari, hasa katika Jiji la Dar es Salaam.

Amesema ajali za barabarani zinaendelea kusababisha vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu, huku watembea kwa miguu, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki na watoto wakiwa makundi yanayoathirika zaidi.

Amesema kuwa, suluhisho la changamoto hiyo ni kuanza kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watoto tangu wakiwa shuleni ili wajue namna sahihi ya kutumia barabara na kuheshimu sheria za usalama.


"Usalama barabarani si jukumu la Jeshi la Polisi pekee, ni wajibu wa kila mmoja wetu, kuanzia Serikali, taasisi, shule, wazazi hadi wananchi kwa ujumla," alisema.

Aidha, amewataka madereva wa vyombo vyote vya usafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuelimisha jamii.

Kwa upande wake, Makamo wa Rais Utawala, AAT Hanif Virji, alisema kupitia FIA Safe and Sustainable Mobility Grant Programme, taasisi hiyo imetekeleza mradi wa usalama barabarani katika shule 19 za msingi na sekondari za Wilaya ya Ubungo.

Amesema mbali na kutoa elimu kwa wanafunzi na walimu, AAT imeboresha miundombinu ya usalama katika maeneo ya shule hizo kwa kuweka alama za barabarani, michoro ya usalama, vivuko vya waenda kwa miguu (zebra crossing) pamoja na matuta ya kupunguza mwendo wa magari.

Ameongeza kuwa, lengo la mradi huo ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapoingia na kutoka shuleni pamoja na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika familia na jamii zao.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibasila, Leticia Pascal Martin, amesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa matumizi sahihi ya barabara na kutambua alama mbalimbali za usalama.

Amesema kuwa, maarifa hayo yatawasaidia wanafunzi kujilinda wanapokuwa barabarani na pia kuwafundisha wazazi, ndugu na jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Aidha, amewataka madereva kuzingatia alama za barabarani na kufuata sheria zote za usalama ili kupunguza ajali ambazo zinaweza kuzuilika.

Mradi huo unatarajiwa kuendelea kuongeza uelewa wa usalama barabarani kwa watoto na kuimarisha ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, AAT, shule na wadau wengine katika juhudi za kupunguza ajali za barabarani nchini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3