MKURUGENZI MTENDAJI,(BUWASA) AONYA WANAOKIUKA MAADILI YA KAZI.
Na Mwandishi wetu, Matukio Daima News.
BUKOBA,KAGERA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), Bw. John Sirati, ametoa onyo Kwa watumishi wa mamlaka hiyo wanaokiuka taratibu za kazi.
Amesema hayo Katika kikao chake na watumishi wa Mamlaka hiyo, kilicholenga kuimarisha ushirikiano, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kujadili mwelekeo wa utekelezaji wa majukumu.
Amesisitiza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya mtumishi yeyote atakayebainika kuhujumu mamlaka au kushirikiana na wateja kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria na kanuni za utumishi.
Bw,Sirati amewataka watumishi kuendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu. na kusema kuwa huduma bora kwa wananchi inapaswa kuwa kipaumbele ili kuhakikisha wateja wanapata huduma za maji safi kwa wakati na kwa viwango.
"Sitasita kumchukulia hatua mtumishi yeyote anayekiuka taratibu za kazi, ikiwemo watumishi wasiowaaminifu wanaoshirikiana na waharifu kuihujumu Mamlaka," amesema Bw. Sirati.
Aidha, amewataka watumishi kuimarisha ushirikiano kati ya idara na vitengo mbalimbali ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu, kufanikisha malengo ya BUWASA na kuendelea kujenga mahusiano mazuri na wateja.
Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kutoa maoni, kuuliza maswali na kuwasilisha mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Pia aliahidi kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyowasilishwa, akieleza kuwa yatasaidia kuimarisha utendaji kazi Wa mamlaka na kuboresha huduma kwa wananchi.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wito kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kudumisha mshikamano na kushirikiana ili kuhakikisha BUWASA inaendelea kutoa huduma bora, endelevu na zinazokidhi matarajio kwa wananchi.



