Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
VIONGOZI TANGA WATAKIWA KUWA MBOGO DHIHI YA RUSHWA

VIONGOZI TANGA WATAKIWA KUWA MBOGO DHIHI YA RUSHWA

 .


NA AMINA SAIDI,

MATUKIO DAIMA TANGA.


​WATUMISHI wa umma, watendaji wa taasisi na wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Tanga wametakiwa kuwa walinzi wakali wa fedha za umma kwa kuziba mianya yote ya rushwa na ubadhirifu, ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inawafikia wananchi ikiwa na ubora unaostahili.


​Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, wakati akifungua warsha ya wadau wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo, iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).


​Akizungumza katika warsha hiyo, Nyamwese alisisitiza kuwa rushwa ni adui mkuu anayedhoofisha ubora wa miradi, kuongeza gharama zisizo na msingi na hatimaye kumnyima mwananchi haki ya kupata huduma bora na kubomoa imani yake kwa serikali.


​"Hatuwezi kufikia malengo ya maendeleo tuliyojiwekea kwenye Dira ya Taifa ya 2050 ikiwa tutaruhusu rushwa na ubadhirifu vitawale.


 Mapambano haya si ya TAKUKURU pekee, bali ni wajibu wa kila kiongozi na mtumishi katika eneo lake," alisisitiza Nyamwese.


​Alieleza kuwa Serikali kuu inautazama Mkoa wa Tanga kama kitovu cha biashara na uwekezaji kutokana na fursa za kimkakati kama vile mradi wa Bomba la Mafuta, ujenzi wa barabara kuu ya Tanga–Dar es Salaam, na uboreshaji wa Bandari ya Tanga.

​Nyamwese alibainisha kuwa takriban Shilingi Trioni 3.17 zimepelekwa mkoani humo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, na kwamba fedha hizo hazitakuwa na maana kama wasimamizi wa miradi hawatatenda kazi zao kwa uzalendo, weledi na uaminifu mkubwa.


​Kwa upande wake, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah, alisema tathmini iliyofanywa na taasisi hiyo kwenye miradi mbalimbali ilibaini uwepo wa changamoto za usimamizi mbovu, ucheleweshwaji wa utekelezaji na matumizi yasiyo sahihi ya fedha.


​Ndwatah alieleza kuwa lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kukumbushana wajibu wao wa kisheria na kimaadili, huku akiwataka kuongeza ushirikiano na TAKUKURU ili kulinda rasilimali za umma na kuhakikisha wananchi wanapata thamani halisi ya fedha zilizowekezwa. 



​Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kupitia Tamisemi kuangalia upya makadirio ya vifaa vya ujenzi  kwenye miradi, ili ziendane na uhalisia wa bei za sokoni wakati wa utekelezaji.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3