UMOJA WA MAFUNDI SIMU NA WAUZAJI SIMU NA KOPYUTA IRINGA (UWAMASICI ) WAZINDULIWA KWA KISHINDO
DAS Iringa Bernard Urassa akizindua vitambulisho vya wanachama wa UWAMASICI
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.
Umoja wa Wauzaji na Mafundi Simu na Kompyuta Mkoa wa Iringa (UWAMASICI) umeshauriwa kuzingatia maadili ya kazi kwa kufanya shughuli zao kwa weledi, uaminifu na kuwahudumia wateja kwa ubora, na kuwa sifa ya fundi bora ni kutoa huduma zinazozingatia sheria na taratibu, huku akiwataka kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya taaluma yao.
DAS Iringa Bernard Urassa akizindua sare ya UWAMASICIAkizungumza wakati wa uzinduzi wa umoja huo uliofanyika katika Ukumbi wa Lugalo mjini Iringa, mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa Renjamini Urassa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Benjamini Sitta alisema kuwa umoja huo ni fursa muhimu ya kupata viongozi watakaosimamia maslahi ya wanachama na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa mitaji, mafunzo ya kitaalamu na fursa za kukuza biashara.
Urassa aliwataka mafundi simu kuzingatia maadili ya kazi kwa kufanya shughuli zao kwa weledi, uaminifu na kuwahudumia wateja kwa ubora, alisisitiza kuwa sifa ya fundi bora ni kutoa huduma zinazozingatia sheria na taratibu, huku akiwataka kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya taaluma yao.
“Serikali inaendelea kutambua mchango wa vijana katika maendeleo ya uchumi kupitia vikundi mbalimbali hivyo kuwataka wanachama wa UWAMASIC kutumia fursa za mafunzo, mikopo na programu mbalimbali za uwezeshaji. Pia niwahimize kuendelea kulinda amani ya nchi na kutumia umoja huu kama chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi”alisema
Aidha mwakilishi wa Jeshi la Polisi aliwataka mafundi na wafanyabiashara wa simu kujiepusha na kupokea, kununua au kuuza simu na vifaa vya mawasiliano vinavyoshukiwa kuwa vya wizi, likisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai linaloweza kusababisha mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema wafanyabiashara wanapaswa kuwa waangalifu wanaponunua simu kutoka kwa wateja, hasa pale kifaa kinapouzwa kwa bei isiyoendana na thamani yake halisi. Alisema endapo fundi atahisi simu ni ya wizi, anatakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi badala ya kuikubali.
“Jeshi la Polisi linawalionya mafundi dhidi ya kufungua (kuflashi) simu ambazo mwenye nazo hana uthibitisho wa umiliki au amesahau nywila kwa mazingira yanayotia shaka,kwa sababu huduma hiyo inaweza kusaidia kuficha ushahidi wa uhalifu na kumfanya fundi ahusishwe na makosa ya jinai”
Jeshi hilo lilisisitiza kuwa lipo tayari kulinda usalama wa watu watakaotoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na kwamba ushirikiano wa mafundi simu utasaidia kupunguza matukio ya wizi wa simu pamoja na uhalifu mwingine unaohusisha vifaa vya mawasiliano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa nidhamu katika umoja huo Abubakar Sadick alisema umoja huo umeanzishwa kutasaidia kupunguza matukio ya wizi wa simu, kuimarisha uwajibikaji wa mafundi na kuongeza ulinzi kwa wateja wanaopata huduma za matengenezo ya simu na kompyuta.
Sadick alisema umoja huo umeanzishwa ukiwa na dhamira ya kuwaunganisha mafundi na wauzaji wa simu pamoja na kompyuta, kulinda maslahi yao na kuboresha huduma kwa wananchi huku ukichangia kupunguza matukio ya wizi wa simu na utapeli katika sekta hiyo.
Abubakar alisema kuanzishwa kwa umoja huo kumetokana na hitaji la kuwa na chombo kitakachowaleta pamoja mafundi na wauzaji ili kusaidiana wanapopata changamoto, kujenga mshikamano na kusimamia maadili ya kazi huku kila mwanachama ametambuliwa kwa kitambulisho rasmi ili wananchi waweze kutofautisha mafundi halali na wasiokuwa wanachama wa umoja huo.
“Kila mwanachama wa UWAMASICI atakuwa na kitambulisho rasmi kitakachomtambua, hatua hiyo itawasaidia wananchi kutofautisha mafundi waliohalali na wasiokuwa wanachama wa umoja huo. Aliwataka wateja kuomba kuona kitambulisho cha fundi kabla ya kukabidhi simu zao kwa matengenezo”alisema
“Wananchi wanashauriwa kumuomba fundi kitambulisho chake kabla ya kumpatia simu kwa matengenezo, hatua itakayosaidia kujenga uaminifu na kurahisisha uwajibikaji endapo kutatokea malalamiko ya wateja na kushirikiana na vyombo vya dola katika kubaini simu zinazoshukiwa kuwa za wizi au zinazohusishwa na vitendo vya uhalifu”alisema
Aidha, alisema UWAMASICI umeweka kanuni za nidhamu kwa wanachama wake na kwamba wanaokiuka taratibu za umoja huchukuliwa hatua kwa mujibu wa katiba na kanuni zilizowekwa ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa zenye ubora na uadilifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja huo Daudi Ulenge alieleza kuwa mbali na kutetea maslahi ya wanachama,UWAMASICI pia imejipanga kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu na kuendesha shughuli za kijamii kila mwaka.
Viongozi hao pia waliiomba Serikali kuendelea kuwawezesha vijana waliojiajiri kupitia mikopo na fursa mbalimbali za maendeleo ili waweze kuanzisha miradi ya pamoja itakayouimarisha umoja huo na kuongeza ajira kwa vijana mkoani Iringa.
Aidha uzinduzi wa umoja huo ulihudhuriwa na mamia ya mafundi na wauzaji wa simu pamoja na kompyuta kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa, huku viongozi wakieleza kuwa UWAMASICI unatarajiwa kuwa kiungo muhimu kati ya watoa huduma, wananchi na taasisi za serikali katika kuhakikisha huduma za matengenezo na biashara ya simu zinafanyika kwa uadilifu, uwajibikaji na kuzingatia sheria.
</
p>





















































































































