Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MKULIMA BORA 2024 ACHOCHEA MAPINDUZI YA UZALISHAJI WA PAMBA CHATO.

MKULIMA BORA 2024 ACHOCHEA MAPINDUZI YA UZALISHAJI WA PAMBA CHATO.

 


Na CHAUSIKU SAID_MATUKIO DAIMA.

Kupatikana kwa mkulima bora wa zao la pamba nchini mwaka 2024, Walwa Zacharia Malimi kumegeuka kuwa chachu ya kuongeza uzalishaji wa pamba katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita, huku wakulima wengine wakiachana na  mfumo wa kilimo cha mazoea na kuanza kutumia kanuni za kilimo bora.


Walwa, ambaye alitunukiwa trekta na Serikali kutokana na mafanikio yake katika uzalishaji wa pamba, amesema mafanikio hayo yalianza baada ya kupata mafunzo ya kilimo bora kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa na Bodi ya Pamba. 


Kupitia mafunzo hayo aliyoyapata alianza kulima kwa kutumia vipimo vya sentimita 60 kwa 30 pamoja na matumizi sahihi ya mbolea, hatua iliyoongeza mavuno kwa kiwango kikubwa, awali kabla ya kupokea elimu hiyo alieleza kuwa alikuwa akivuna kati ya kilo 500 hadi 600 kwa ekari moja lakini baada ya kuzingatia kanuni za kilimo bora mavuno yaliongezeka kilo 2,700 mpaka kufikia  kilo 2,900 msimu uliofuata, huku mwaka huu akitarajia kuvuna zaidi ya kilo 3,000 kwa ekari moja.



Walwa amesema tuzo ya trekta aliyopata imeimarisha zaidi uzalishaji wake na kubadilisha maisha yake kiuchumi, huku akisisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuachana na kilimo cha mazoea na kukumbatia teknolojia mpya pamoja na ushauri wa wataalamu wa kilimo.


 Musa Joseph ni Mkulima wa Kijiji cha Songambele amesema mafanikio ya Walwa yaliwapa hamasa wakulima wengi waliokuwa wamekata tamaa ya kulima pamba kutokana na mavuno duni ya kilo 150 hadi 170 kwa ekari, lakini baada ya kuona matokeo hayo chanya  wakulima wengi wamebadili mfumo wa uzalishaji na sasa wanapata mavuno makubwa zaidi.


Naye mkulima Philipo Kanyerere amesema awali walihofia mfumo mpya wa upandaji wa sentimita 60 kwa 30 wakidhani pamba ingebanana, lakini baada ya kutumia mbolea kama ilivyoelekezwa walishuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji na kuthibitisha kuwa pamba ni  kilimo bora na chenye tija zaidi.



Afisa Kilimo kutoka  BBT katika Kijiji cha Songambele, Christopher Julius, amesema matokeo ya Walwa yamekuwa ushahidi unaowashawishi wakulima wengi kubadili mtazamo na kuanza kulima kitaalamu, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha kila mkulima anafikia angalau kilo 2,000 kwa ekari.


Kwa upande wake, Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Chato kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Samwel Mdidi, amesema Walwa amekuwa balozi muhimu wa kilimo bora, ambapo hadi sasa anawafundisha zaidi ya wakulima 160.


 Mdidi amesema kuwa mwitikio wa wakulima umeongezeka baada ya kuona matokeo halisi ya uzalishaji, na kwa msimu huu wilaya inatarajia kuzalisha kati ya kilo milioni sita mpaka saba za pamba licha ya changamoto za ukame zilizochelewesha upandaji.



Naye Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Berino Msigwa, amesema halmashauri inaendelea kushirikiana na maafisa ugani kuhakikisha wakulima wanazingatia kanuni za kilimo bora ili kuongeza uzalishaji, kipato cha wakulima na mapato ya halmashauri kupitia zao la pamba.


Mafanikio ya mkulima bora wa mwaka 2024 yanaendelea kuwa mfano wa kuigwa, yakionyesha kuwa matumizi ya teknolojia, elimu ya ugani na uzingatiaji wa kanuni za kilimo bora vinaweza kuongeza uzalishaji wa zao la pamba na kuinua uchumi wa wakulima pamoja na taifa kwa ujumla.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3