Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TAASISI YA USULUHISHI WA KODI YAIMARISHA MAPAMBANO YA MIGOGORO YA KODI

TAASISI YA USULUHISHI WA KODI YAIMARISHA MAPAMBANO YA MIGOGORO YA KODI

 


Matukio DaimaMedia 


Taasisi ya Usuluhishi wa Kodi imewahimiza walipakodi na wananchi kutumia huduma mbalimbali zilizowekwa ili kuwasilisha malalamiko na kupata elimu ya kodi, hatua inayolenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari.


Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba),Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui amesema kwa kipindi cha miaka miwili na nusu tangu kuanzishwa kwake, taasisi imejikita katika kutoa elimu, kupokea na kusuluhisha migogoro ya kodi pamoja na kupokea malalamiko ya wazi na ya siri kutoka kwa wananchi.


Ameeeleza kuwa taasisi imeanzisha njia mbalimbali za kupokea malalamiko ikiwemo mabanda ya maonesho, simu za bure, mfumo wa mtandao, programu ya simu "Suluhu ya Kodi", pamoja na huduma ya USSD kwa watumiaji wa simu zisizo janja ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote.


Kwa mujibu wa taasisi hiyo, katika kipindi cha miaka miwili na nusu imepokea takriban malalamiko 593, huku malalamiko 347 yakitatuliwa kwa mafanikio katika mwaka uliopita pekee.


Aidha, taasisi imeeleza kuwa utoaji wa elimu na usuluhishi wa migogoro ya kodi unalenga kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, pamoja na kuchangia azma ya kukuza uchumi kwa wastani wa asilimia 10 na kufikia uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja.


Taasisi hiyo pia ilitoa shukrani kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa maandalizi mazuri ya Maonesho ya Sabasaba na kuwataka wananchi kutembelea banda lao ili kupata elimu ya kodi na kuwasilisha changamoto zinazowakabili.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3