JKT YAIBUKA KIDEDEA KWA BIDHAA ZA KILIMO NA UVUVI, YAHAKIKISHA KUUNGA MKONO DIRA YA TAIFA 2050
Na Matukio DaimaMedia
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeibuka mshindi wa nafasi ya kwanza katika kundi la bidhaa za kilimo na uvuvi, likieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa katika uzalishaji, mafunzo kwa wananchi na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maonesho ya Sabasaba Kitaifa, JKT Brigedia Jenerali Shija Lupi amesema ushindi huo unaonyesha juhudi za JKT katika kuendeleza sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi, huku akimshukuru Mungu na kuahidi kuendelea kuboresha ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Brigedia Jenerali Lupi ameeleza kuwa JKT inaendesha mashamba makubwa ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, sambamba na kutoa mafunzo ya kilimo na uvuvi kwa wananchi bila malipo ili kuwajengea uwezo wa kuongeza uzalishaji na kipato.
Aidha, amesema JKT imeendelea kuwekeza katika mitambo ya kisasa kupitia kampuni zake, pamoja na kujenga mabwawa ya ufugaji wa samaki, kuanzisha viwanda vya usindikaji na kutekeleza miradi ya ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na ujenzi wa kiwanda cha maziwa.
Ameongeza kuwa, juhudi hizo ni sehemu ya maandalizi ya kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo JKT inalenga kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kuongeza uzalishaji wenye tija, kuimarisha viwanda na kutoa mafunzo yatakayochochea maendeleo ya sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Hata hivyo, amewataka wananchi kutembelea banda la JKT ili kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na jeshi hilo pamoja na kupata elimu kuhusu fursa na teknolojia zinazotumika katika uzalishaji.
Brigedia Jenerali Lupi amesisitiza kuwa JKT itaendelea kuboresha huduma na bidhaa zake ili kuendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri katika maonyesho na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.


