Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ARUSHA KUANDIKA HISTORIA,TAMASHA KUBWA LA SANAA NA UFUNDI OCTOBER 2026

ARUSHA KUANDIKA HISTORIA,TAMASHA KUBWA LA SANAA NA UFUNDI OCTOBER 2026

 


Na Pamela Mollel,Arusha 


Arusha inatarajia kuandika historia mpya kupitia Tamasha kubwa la Sanaa na Kazi za Ufundi litakalofanyika Oktoba mwaka 2026, tukio linalolenga kuipa nguvu sekta ya utalii na sanaa pamoja na kukuza uchumi na ubunifu nchini Tanzania



Tamasha hilo linaandaliwa na Tanzania International Tourism Festival (TITF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TASFA), likiwa limebeba dhamira ya kuwaunganisha wasanii, wabunifu na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi wa TITF, Ibrahim Jamal, amesema lengo kuu la tamasha hilo ni kuinua thamani ya kazi za ubunifu na kuzifanya ziwe na ushindani katika masoko ya kimataifa kupitia sekta ya utalii


Amefafanua kuwa tamasha hilo litakuwa jukwaa muhimu litakalowakutanisha wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mavazi, watengenezaji wa vito, wafinyanzi na wasanii wa kazi za mikono kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania


Mbali na maonesho ya sanaa, washiriki watapata fursa ya mafunzo maalum yatakayojikita katika uongezaji thamani wa bidhaa, ulinzi wa haki miliki za kazi za ubunifu pamoja na mbinu za kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi


Aidha, kutakuwa na maonyesho ya moja kwa moja ya utengenezaji wa kazi za sanaa (live demonstrations) pamoja na mikutano ya kibiashara (B2B) itakayowaunganisha wasanii na wanunuzi wakubwa pamoja na wawekezaji wa kimataifa



Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), Rukia Walele, amesema tamasha hilo linafungua ukurasa mpya kwa sekta ya sanaa za ufundi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikichangia uchumi na kuhifadhi utamaduni wa Kitanzania


Ameongeza kuwa kupitia vyama zaidi ya 20 vinavyounda shirikisho hilo, maelfu ya wasanii nchini watapata nafasi ya kutambulika, kujifunza mbinu za kisasa za biashara na kujenga mitandao itakayowaingiza katika masoko ya kikanda na kimataifa


Aidha, amesema sanaa za ufundi ni nguzo muhimu ya uchumi wa ubunifu, hivyo tamasha hilo litasaidia kuongeza kipato kwa wasanii na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha sanaa na utalii barani Afrika


 Waandaaji wamesisitiza kuwa Arusha itakuwa kitovu cha ubunifu na utalii wakati wa tamasha hilo, ambalo linatarajiwa kuvutia maelfu ya washiriki na wageni kutoka mataifa mbalimbali, ikiwa ni chachu ya mageuzi ya kiuchumi kupitia sanaa na utamaduni.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3