TEKNOLOJIA YA DAWA ZA ASILI YALETA MAPINDUZI KATIKA UCHAKATAJI WA NGOZI
Na Matukio DaimaMedia
Shirika la utafiti na maendeleo ya Viwanda Tanzania (Trido) limekuja na teknolojia mpya ya kutengeneza dawa ya kuchakata ngozi inayotokana na mimea asili, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya kemikali za viwandani kama chrome na kuimarisha afya ya watumiaji pamoja na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza katika maonyesho ya 50 ya biashara ya kimataifa (Sabasaba) kaimu mkuu wa kitengo cha teknolojia za nguo na ngozi Mhandisi Yusufu Sampuli amesema dawa hiyo hutumika katika uchakataji wa ngozi na pia katika utengenezaji wa coating na rangi za bidhaa za ngozi, huku tafiti za kuboresha rangi zinazotokana na mimea na masalia ya kilimo zikiendelea mwaka huu.
Amesema kuwa, soko la bidhaa ambazo zinaongezwa kutoka na vitu asili limeongezeka sana hususani mataifa kama ulaya ambayo yanahitaji bidhaa za ngozi iliyochakatwa kwa mimea asili na siyo kemikali kwani bidhaa zinazotokana na kemikali huhatarisha usalama wa afya ndio maana unaweza ukavaa viatu ukachubuka au ukapata fangasi.
Ameeeza kuwa matumizi ya dawa za asili hupunguza mabaki ya kemikali hatarishi kwenye ngozi zilizochakatwa, jambo linalosaidia kulinda afya za wazalishaji, watumiaji na mazingira kwa ujumla.
Mhandisi Sampuli amesema, mahitaji ya bidhaa za ngozi zilizochakatwa kwa njia rafiki kwa mazingira yanaendelea kuongezeka katika soko la kimataifa, hususan nchi za Ulaya, huku baadhi ya wajasiriamali wa mkoa wa Kilimanjaro tayari wakianza kutumia teknolojia hiyo na kupata matokeo chanya.
Aidha, amesema teknolojia hiyo imefungua fursa mpya za ajira kupitia kilimo cha mimea inayotumika kutengeneza dawa za kuchakata ngozi, uchakataji wa ngozi ghafi pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za ngozi zenye thamani kwa soko la ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa, shirika linaendelea kufanya ziara za ufuatiliaji kwa wajasiriamali ili kutathmini maendeleo, kutatua changamoto na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa ufanisi.
Aidha, amewataka wananchi na wajasiriamali wanaohitaji kutumia teknolojia hiyo wanahimizwa kuwasiliana na shirika kupitia simu, barua pepe au ofisi zake kwa ajili ya kupata maelekezo na huduma za kitaalamu.
Sambamba na hilo, amesema kuwa tafiti zitaendelea kuboresha ubora wa dawa, rangi na coating zinazotokana na vyanzo vya asili, kwa lengo la kuongeza ajira, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira huku Tanzania ikizalisha bidhaa za ngozi zinazoweza kushindana katika masoko ya kimataifa.

