DEFENDDEFENDERS YAIJENGEA UWEZO MISA TANZANIA KATIKA USALAMA WA KIDIJITALI
Na Matukio Daima Media
Shirika la DefendDefenders la Uganda limeendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha uwezo wa taasisi zinazotetea haki na uhuru wa vyombo vya habari kwa kuikabidhi Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania,MISA Tanzania, vifaa vya teknolojia vinavyolenga kuongeza ufanisi wa utendaji na kuimarisha usalama wa kidijitali.
Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika leo Julai 23, 2026, katika Ofisi za MISA Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo mwakilishi wa DefendDefenders, John Kaoneka, alikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa MISA Tanzania.
Miongoni mwa waliokuwepo katika makabidhiano hayo ni Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, Makamu Mwenyekiti, Rhoda Marumo, pamoja na Afisa Utawala, Glory Kalinga.
Msaada huo umejumuisha laptop, kamera za CCTV, simu ya mkononi, router, external hard drive, Seagate backup drive, ESET Smart Security na Wi-Fi SIM Card.
Kwa mujibu wa MISA Tanzania, vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ulinzi wa taarifa na mifumo ya kidijitali ya taasisi, kuboresha mawasiliano na kuimarisha uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na usalama wa wanahabari.
MISA Tanzania imesema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano unaoendelea kati yake na DefendDefenders, huku ikieleza kuwa vifaa hivyo vitatumika kwa uwazi na uwajibikaji katika kuimarisha utendaji wa taasisi na huduma kwa wanachama.
Taasisi hiyo imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mazingira salama kwa wanahabari na kulinda uhuru wa vyombo vya habari nchini.


