Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ASIA ABDALLAH AWAONYA WANACHAMA KUEPUKA MAJUNGU, UKABILA NA MIGAWANYIKO

ASIA ABDALLAH AWAONYA WANACHAMA KUEPUKA MAJUNGU, UKABILA NA MIGAWANYIKO


Na Hamida RamadhanMatukio Daima Media, Dodoma

MJUMBE wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Taifa (UWT) kutokea Mkoa wa Dodoma, Asia Abdallah, amezindua Umoja wa Leo Yetu Kesho Yetu huku akiwataka wanachama wake kudumisha mshikamano, kuepuka majungu, ubinafsi na migawanyiko inayoweza kudhoofisha umoja huo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma, Asia ambaye amewahi Kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa alisema mafanikio ya umoja huo yatategemea zaidi ushirikiano, uaminifu na uwezo wa wanachama kufanya kazi kwa pamoja bila kuruhusu tofauti za kisiasa, kikabila au kidini kuwagawa.

Amesema taasisi za kifedha na mabenki zina nafasi kubwa ya kusaidia vikundi na jumuiya za kijamii na kiuchumi kukua, lakini mafanikio hayo hayawezi kupatikana ikiwa kutakuwa na migogoro ya ndani miongoni mwa wanachama.

“Tunayo kazi ya pamoja ya kufanya na mabenki ili kuviinua vikundi hivi. Nasaha zangu kwenu ni kuhakikisha hamuendelezi majungu, ubinafsi wala migawanyiko. Umoja usiofungamana na makundi yenye maslahi binafsi utakuwa na nguvu kubwa ya kuleta maendeleo,” amesema Asia.

Ameongeza kuwa wanachama wanapaswa kuwa makini dhidi ya watu au makundi yenye dhamira ovu yanayoweza kujaribu kuvuruga mshikamano wao kwa kutumia siasa, ukabila au misingi ya kidini.

“Mkiendelea kushikamana na kulinda misingi yenu, nina imani mtazalisha mamilionea na hata mabilionea. Kadri umoja huu unavyokua, ninaona mwakani utakuwa na mafanikio makubwa zaidi ya kifedha,” amesema.

Asia amewataka wanachama kuweka uzalendo mbele, kuwa wavumilivu wanapokutana na changamoto na kuepuka kufanya maamuzi kwa haraka au kwa hasira. 

Amesema uongozi wa watu ni jukumu gumu linalohitaji hekima na uvumilivu, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuunga mkono viongozi wao ili kuimarisha usalama wa taifa na maendeleo ya nchi.

“Mkiona chokochoko au dalili za vurugu, wasilianeni na viongozi wa maeneo yenu. Hakuna maendeleo yatakayopatikana ikiwa kutakuwa na vurugu. Tusikubali mtu yeyote kutugawa,” amesema Asia

Aidha, Asia amewahakikishia wanachama kuwa yuko tayari kuendelea kushirikiana nao na kutumia uzoefu wake kusaidia maendeleo ya umoja huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja huo,Remigius Mubago, amesema umoja huo ulianza kwa maono ya wanachama mwaka 2024 na kuanza rasmi tarehe 27 Agosti mwaka huo ukiwa na wanachama 52.

Amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa umoja huo ni kujenga mshikamano, kusaidiana katika nyakati za shida na furaha pamoja na kuwajengea wanachama uwezo wa kiuchumi ili kupunguza utegemezi.

“Mtazamo wa jina letu ni kwamba ustawi wa kesho unaanza na maandalizi ya leo. Huu ni umoja wa hiari unaolenga kuwakutanisha watu kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kusaidiana na kuendelezana,” amesema Mubago.

Ameeleza kuwa miongoni mwa malengo ya umoja huo ni kusaidia wanachama wanapokumbwa na majanga au misiba, kuanzisha na kuendesha miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha hali za maisha za wanachama wake.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Mubago amesema umoja huo umefanikiwa kusimamia ukusanyaji wa michango, ada na mifuko ya kusaidia wanachama wakati wa misiba na changamoto mbalimbali.

Amesema hadi sasa jumla ya wanachama 19 wamenufaika na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi zenye thamani ya shilingi milioni 27.9, huku idadi ya wanachama ikiongezeka kutoka 52 hadi kufikia 120.

Hata hivyo, amesema bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanachama kushindwa kufuata taratibu za umoja na wengine kujiondoa wenyewe pamoja na ukosefu wa vitendea kazi muhimu vya kuendeshea shughuli za kila siku.

Mubago amesema matarajio yao ni kupata ardhi kwa ajili ya kujenga ofisi za umoja, kununua basi aina ya Coaster pamoja na viti na matenti kwa matumizi ya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Amesema mahitaji hayo yanakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 124 na yatasaidia umoja huo kuwa na vitega uchumi na mali zake wenyewe, hatua ambayo itapunguza gharama za uendeshaji na kuongeza mapato.

Kutokana na imani waliyonayo kwa mchango wake katika maendeleo ya jamii, wanachama wa umoja huo walimuomba Asia Abdallah kukubali kuwa mlezi wa umoja huo ambapo alikubali.

Mwisho


 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3