NDEJEMBI ATOA AGIZO ZITO MRADI WA CHALINZE–DODOMA UKIKARIBIA MWISHO
Matukio Daima, Morogoro
WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameagiza mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu mkoani Dodoma kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa wakati ili Watanzania waanze kunufaika na huduma ya umeme yenye uhakika.
Agizo hilo linakuja wakati mradi huo wa kilometa 345 ukiwa umefikia asilimia 89 ya utekelezaji na ukitarajiwa kukamilika Agosti 21 mwaka huu.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Morogoro, Ndejembi amesema Serikali haitaki kuona ucheleweshaji wa mradi huo kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha usafirishaji wa umeme kutoka vyanzo vikubwa vya uzalishaji kwenda maeneo yenye mahitaji makubwa ya nishati.
Amesema mradi huo utaongeza uwezo wa Gridi ya Taifa kusafirisha umeme unaozalishwa katika Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere na hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na maeneo mengine.
"Nchi inaendelea kukua kiuchumi na mahitaji ya umeme yanaongezeka kila siku. Ndiyo maana tunasisitiza mradi huu ukamilike kwa wakati ili wananchi na wawekezaji wapate huduma ya uhakika," amesema.
Pia ameitaka TANESCO na mkandarasi kushughulikia haraka changamoto zote zinazoweza kuathiri kasi ya utekelezaji wa mradi, ikiwemo tofauti zinazojitokeza kati ya watumishi wa kampuni ya TBEA na wafanyakazi wa mradi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Serikali inaendelea kuona matokeo ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya umeme, huku wananchi wengi zaidi wakiendelea kuunganishiwa huduma hiyo.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, shirika hilo limeandika historia kwa kuunganisha zaidi ya wateja laki nane, hatua inayoonyesha ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme na mafanikio ya miradi ya miundombinu inayotekelezwa nchini.
Kwa mujibu wa Twange, kila mteja mpya anayepata umeme anachochea ukuaji wa biashara, uzalishaji wa viwandani, utoaji wa huduma za afya na elimu pamoja na kuboresha kipato cha wananchi.
Naye Meneja wa Mradi, Newton Mwakifwamba, amesema kazi zinaendelea vizuri katika maeneo yote ya mradi na kwamba mkandarasi anaendelea na hatua za mwisho za utekelezaji ili kukidhi ratiba ya mkataba.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuongeza ufanisi wa Gridi ya Taifa na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya Watanzania.

