MANISPAA YA IRINGA YAVIWEZESHA VIKUNDI MIKOPO ISIYO NA RIBA TSH MILIONI 420 .
Mkuu wa wilaya ya Iringa Benjamin Sitta (mwenye suti nyeusi) katikati akiwa na mbunge wa Iringa mjini Fadhil Ngajilo kulia kwake ,mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada kushoto kwake na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Zaina Mlawa wanne kutoka kushoto jana wakati wa kukabidhi mikopo zaidi ya Tsh milioni 400 kwa vikundi picha na Matukio Daima Media
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa inaendelea kutekeleza kwa vitendo sera ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia matumizi ya sehemu ya mapato yake ya ndani, ambapo wananchi 124 walioungana katika vikundi vya ujasiriamali wanatarajia kunufaika na mkopo wenye thamani ya Shilingi milioni 420.
Mikopo hiyo inalenga kuyawezesha makundi mbalimbali ya kijamii kuongeza mitaji, kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wanufaika, kuchochea ajira na kukuza uchumi wa familia pamoja na maendeleo ya Manispaa kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Iringa Benjamin Sitta akiwaendesha mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada kutoka kushoto ,mkurugenzi Manispaa ya Iringa Zaina Mlawa na mbunge wa Iringa mjini Fadhil Ngajilo leo wakati wa kukabidhi bajaji ,pikipiki na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 420 kwa vikundiHayo yamesema na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa wakati akizungumza na wananchi hao waliojitokeza kwa ajili ya kupewa elimu ya matumizi bora ya fedha hiyo ya mkopo.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhakikisha mapato ya ndani yanatumika kwa tija, hususan katika kuwawezesha wananchi kujitegemea kiuchumi kupitia vikundi vya ujasiriamali vinavyotekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza Meya wa Manspaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema Halmashauri itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mikopo inayotolewa kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuhakikisha inawanufaisha walengwa na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, alimpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na timu ya menejimenti kwa ushirikiano na kujituma katika kusimamia miradi na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ndiyo msingi wa mafanikio yanayopatikana katika halmashauri.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini amewataka wananchi kuendelea kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kwa kuchangia kile wanachoweza, akisisitiza kuwa msaada haupimwi kwa ukubwa wake bali kwa nia ya kumuinua anayehitaji.
Alisema watu wanaopokea misaada wanapaswa kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili iweze kuwaletea maendeleo ya kudumu. Alibainisha kuwa baadhi ya wanufaika wamekuwa wakitumia fedha kinyume na makubaliano, jambo linalopunguza ufanisi wa programu za uwezeshaji.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa maboresho ya mifumo ya utoaji wa mikopo kwa makundi maalumu, akieleza kuwa hatua ya kuruhusu hata mtu mmoja mmoja kunufaika na mikopo badala ya kulazimika kuwa kwenye vikundi itaongeza fursa kwa walengwa wengi zaidi.
Mbunge huyo alisema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imeamua kujenga vibanda vya kisasa katika eneo la Posta kwa ajili ya wafanyabiashara wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya kumuunga mkono Rais katika juhudi za kuwawezesha kiuchumi wananchi wenye mahitaji maalumu.
“Nasisitiza umuhimu wa elimu ya ujasiriamali, akieleza kuwa pamoja na uwepo wa mikopo, wananchi wanahitaji maarifa ya kuendesha biashara ili waweze kujitegemea na kuboresha maisha yao”alisema
Aliongeza kuwa kwa wale watakaoshindwa kupata mitaji, serikali na wadau wataendelea kuwasaidia kutafuta fursa mbalimbali za kifedha ili waweze kuanzisha au kukuza shughuli za kiuchumi.
“Takwimu zinaonyesha kiwango cha umaskini nchini kimeendelea kupungua katika miaka ya hivi karibuni, nasisitiza kuwa njia bora ya kuendelea kupunguza umaskini ni kuwajengea wananchi uwezo kupitia elimu ya ujasiriamali, uwezeshaji wa kiuchumi na upatikanaji wa mitaji” alisema Ngajilo
Mwakilishi wa watu wenye ulemavu, Athumani Hamiss ametoa shukrani kwa Mbunge kwa kuwapatia msaada wa usafiri utakaowawezesha kushiriki maadhimisho ya Siku ya Watu wenye Ulemavu Duniani.
Alisema msaada huo utawasaidia kufika kwenye maadhimisho yatakayofanyika kuanzia tarehe 3 hadi 5, na kwamba ni mchango mkubwa katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika shughuli hizo muhimu.
"Tunamshukuru Mbunge kwa kutuunga mkono na kugharamia safari yetu. Msaada huu umetupa fursa ya kushiriki maadhimisho hayo kwa urahisi, na tunathamini sana ushirikiano huu," alisema Smani Jili.
Aliongeza kuwa watu wenye ulemavu wanaendelea kuishukuru Serikali na wadau mbalimbali wanaowaunga mkono katika juhudi za kuhakikisha wanapata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo.

