Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
ALLIANCE LIFE ASSURANCE YAZINDUA OFISI DODOMA, TIRA YATAJA LENGO LA SEKTA YA BIMA KUCHANGIA ASILIMIA 3 YA PATO LA TAIFA

ALLIANCE LIFE ASSURANCE YAZINDUA OFISI DODOMA, TIRA YATAJA LENGO LA SEKTA YA BIMA KUCHANGIA ASILIMIA 3 YA PATO LA TAIFA

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma

KAMPUNI ya Alliance Life Assurance imezindua ofisi yake mpya ya mauzo jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua wigo wa huduma zake na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi pamoja na taasisi mbalimbali.

Hatua hiyo pia inalenga kuongeza matumizi ya huduma za bima nchini na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza mchango wa sekta ya bima katika uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Mipango na Utafiti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Edgar Shao, aliyemwakilisha Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, alisema Serikali inalenga sekta ya bima kuchangia asilimia 3 ya Pato la Taifa (GDP) ifikapo mwaka 2030.

"Kwa sasa sekta ya bima inachangia asilimia 2.18 ya Pato la Taifa, hali inayoonyesha kuwa Tanzania ipo katika mwelekeo mzuri wa kufikia lengo la Serikali la kufikisha mchango huo hadi asilimia 3 ifikapo mwaka 2030," alisema Shao.

Aliongeza kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kunategemea ushiriki mkubwa wa wananchi katika kutumia huduma za bima, huku akisisitiza kuwa huduma hizo ni muhimu katika kulinda maisha, mali na biashara dhidi ya majanga na hasara zisizotarajiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bancassurance wa Alliance Life Assurance, Tumaini Pyanisa, alisema kufunguliwa kwa ofisi hiyo jijini Dodoma ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kusogeza huduma karibu na wateja na kuongeza upatikanaji wa bidhaa mbalimbali za bima.

"Uwepo wa ofisi hii utarahisisha wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma za bima kwa haraka na kwa urahisi zaidi, sambamba na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika maendeleo ya kiuchumi," alisema Pyanisa.

Uzinduzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za bima katika Jiji la Dodoma na maeneo ya jirani, huku ukiunga mkono juhudi za Serikali na wadau wa sekta ya bima katika kuongeza ushiriki wa wananchi na kukuza mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi wa taifa.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3