ALLIANCE LIFE ASSURANCE YASEMA OFISI MPYA DODOMA KUSOGEZA HUDUMA ZA BIMA KARIBU NA WANANCHI
Jul 1, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma
Mkuu wa Kitengo cha Bancassurance wa Alliance Life Assurance, Tumaini Pyanisa, amesema kufunguliwa kwa ofisi mpya ya mauzo ya kampuni hiyo jijini Dodoma kutarahisisha upatikanaji wa huduma za bima na kuzisogeza karibu zaidi na wananchi pamoja na wadau mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo, Pyanisa alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kupanua mtandao wa huduma zake nchini ili kuwafikia wateja wengi zaidi na kuongeza matumizi ya huduma za bima.
"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za bima kwa urahisi zaidi, huku tukiongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda maisha, mali na biashara zao," alisema Pyanisa.
Aliongeza kuwa Alliance Life Assurance itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwemo sekta ya benki kupitia huduma za bancassurance, ili kuhakikisha bidhaa za bima zinawafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mipango na Utafiti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Edgar Shao, aliyemwakilisha Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, alisema Serikali inalenga sekta ya bima kuchangia asilimia 3 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030.
"Kwa sasa sekta ya bima inachangia asilimia 2.18 ya Pato la Taifa, na tunahimiza wananchi kuendelea kutumia huduma za bima ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa," alisema Shao.
Alisema TIRA itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kwa kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma hizo na kuweka mazingira bora yatakayochochea ukuaji wa sekta hiyo nchini.





