Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MUDA WA UWASILISHAJI KAZI TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS  KWA WAANDISHI WAONGEZWA

MUDA WA UWASILISHAJI KAZI TUZO ZA SAMIA KALAMU AWARDS KWA WAANDISHI WAONGEZWA


 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUONGEZWA KWA MUDA WA KUPOKEA KAZI ZA KUSHINDANISHWA KATIKA SAMIA KALAMU AWARDS 2026

Dar es Salaam, Juni 30, 2026

Kamati ya Maandalizi ya Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, inautaarifu umma na wadau wa sekta ya habari na utangazaji nchini kwamba muda wa kupokea kazi za kushindanishwa katika Samia Kalamu Awards 2026 umeongezwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia tarehe 1 Julai 2026 hadi tarehe 14 Julai 2026 saa 5:59 usiku. Awali, muda wa kuwasilisha kazi ulitarajiwa kuhitimishwa tarehe 30 Juni 2026. 

Hata hivyo, kamati imefikia uamuzi wa kuongeza muda kutokana na maombi yaliyowasilishwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji walioomba kupewa muda wa nyongeza ili kukamilisha na kuwasilisha kazi zao ili washiriki kikamilifu katika mashindano haya.

Kamati inawahimiza waandishi wa habari, wahariri, wachora katuni, maafisa habari, watengeneza maudhui ya kidijitali na washiriki wengine wote wenye sifa ambao bado hawajawasilisha kazi zao kutumia kikamilifu muda huu wa nyongeza. 

Maelezo kuhusu makundi ya tuzo, vigezo vya ushiriki na namna ya kuwasilisha kazi yanapatikana kupitia: https://samiaawards.tz/

KUHUSU SAMIA KALAMU AWARDS (SKA)

Samia Kalamu Awards (SKA) ni jukwaa maalumu la kitaifa lililoanzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kutambua, kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na makala za maendeleo nchini. 

Tuzo hizi zinaratibiwa kwa ushirkiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).

Kupitia kaulimbiu ya "Kalamu kwa Maendeleo", Samia Kalamu Awards inalenga kuhimiza uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora, yanayozingatia utafiti, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, sambamba na kutambua mchango wa waandishi wa habari na vyombo vya habari katika kuhabarisha umma kuhusu maendeleo ya Taifa na kuimarisha taswira chanya ya Tanzania ndani na nje ya nchi.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3