Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 WAZEE CHADEMA WAKUTANA SINGIDA KUTOA MWELEKEO WA CHAMA

WAZEE CHADEMA WAKUTANA SINGIDA KUTOA MWELEKEO WA CHAMA


MatukioDaima, Singida,

‎‎Baraza la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAZECHA) Taifa limeanza mkutano wake mkuu wa siku mbili mkoani Singida, ukiwakutanisha wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kujadili masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa chama. Mkutano huo unalenga kuimarisha ushiriki wa wazee katika kutoa ushauri kwa viongozi wa chama kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa, sambamba na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika mazingira ya sasa ya kisiasa.

‎‎Akifungua mkutano huo katika Ukumbi wa Aque mjini Singida, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, aliwataka wajumbe kutumia nafasi hiyo kutoa mawazo na mapendekezo yatakayosaidia kukijenga chama na kuongeza ufanisi wa viongozi wake. Alisema mkutano huo pia utatoa fursa kwa wazee kujikumbusha majukumu yao ya kikatiba na kujadili mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza katika kipindi cha hivi karibuni ndani ya chama.


‎‎Kwa mujibu wa viongozi wa CHADEMA, mkoa wa Singida umechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kama ishara ya mshikamano wa wanachama wa chama hicho. Aidha, mkutano huo umeelezwa kuwa sehemu ya kuonyesha sapoti kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye anaendelea kushikiliwa gerezani akituhumiwa kwa kosa la uhaini. Wajumbe wa mkutano huo pia walifanya maombi maalumu wakimwombea afya njema na kurejea kuendelea na majukumu yake ya kisiasa.‎

Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa, Suzan Lyimo, amesema siku ya pili ya mkutano itahusisha kikao cha kikatiba kitakachotoa mapendekezo na ushauri kwa viongozi wa chama kuhusu masuala mbalimbali yanayolikabili taifa na chama. Amesema ushauri huo utatolewa kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA na utalenga kusaidia viongozi kufanya maamuzi yenye manufaa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

‎‎Naye Mjumbe wa BAZECHA kutoka Pemba, Mohammed Ali Salim, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unatoa nafasi kwa wazee kujadili mustakabali wa chama na kuwasilisha mapendekezo yao kwenye Kamati Kuu ya CHADEMA. Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Maro Maro, amesema elimu na mafunzo yatakayotolewa katika mkutano huo yatawawezesha wazee kuendelea kuelimisha jamii kuhusu uzalendo, haki za wananchi na umuhimu wa kuboresha huduma za afya kwa wazee nchini.


‎MWISHO.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3