Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TOSCI YAWATAKA WAFANYABIASHARA WA MBEGU KUZINGATIA SHERIA NA VIWANGO VYA UBORA

TOSCI YAWATAKA WAFANYABIASHARA WA MBEGU KUZINGATIA SHERIA NA VIWANGO VYA UBORA

 

Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

TAASISI ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imewataka wafanyabiashara wa mbegu nchini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za biashara ya mbegu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na zilizoidhinishwa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao.

Wito huo umetolewa na Mkaguzi wa Mbegu wa TOSCI, Shamba Mapalala, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea jijini Dodoma.

Amesema uzingatiaji wa sheria za biashara ya mbegu ni muhimu katika kulinda maslahi ya wakulima dhidi ya mbegu zisizo na ubora ambazo zinaweza kusababisha hasara mashambani na kupunguza mavuno.

“Tunawaomba wafanyabiashara wa mbegu kuendelea kufuata sheria na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha mbegu zinazowafikia wakulima zimehakikiwa na kuthibitishwa ubora wake. Hii itasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini,” amesema Mapalala.



Amesema sambamba na kuwasimamia wafanyabiashara, TOSCI inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora zilizoidhinishwa na taasisi hiyo.


Mapalala amesema wakulima wanapaswa kununua mbegu zilizowekwa katika vifungashio rasmi vyenye nembo ya TOSCI badala ya kununua mbegu kutoka vyanzo visivyoaminika, ili kuepuka kupata mbegu feki au zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.


Ameeleza kuwa matumizi ya mbegu bora huchangia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha ubora wa mavuno na kuongeza kipato cha wakulima, huku yakichochea ukuaji wa sekta ya kilimo nchini.


Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu bandia ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mapema.


Amesisitiza kuwa matumizi ya mbegu bora na usimamizi madhubuti wa biashara ya mbegu ni miongoni mwa nguzo muhimu za kufanikisha maendeleo ya sekta ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata matokeo bora kutoka katika shughuli zao za uzalishaji.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3