SERIKALI YAONYA WANAOKIUKA MIKATABA YA MABAHARIA
Jun 23, 2026
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
SERIKALI imewataka wamiliki wa meli na makampuni yanayoshughulisha na usafiri na usafirishaji majini kuzingatia mikataba wanayoingia na mabaharia ikiwemo kuzingatia maslahi yao na kuweka mazingira mazuri ya kazi yatakayowezesha mabaharia kutekeleza majukumu yao bila manyanyaso wala ubaguzi.
Katibu Mkuu wizara ya ujenzi na uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ally Saidi alisema hayo mjini Kigoma katika ufunguzi wa maadhimisho ya 16 ya siku mabaharia duniani akimwakilisha Waziri wa ujenzi na uchukuzi wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk.Khalid Mohamed.
Saidi alisema kuwa serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya unyanyasaji unaofanywa kwa mabaharia wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo kunyimwa mishahara yao, kushushwa kwenye meli na kutekelekezwa nj ya nchi bila msaada wowote na stahiki zao nyingine ambazo zinawafanya mabaharia hao na familia zao kuishi maisha magumu.
Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo Kaimu Meneja wa mafunzo na utoaji vyeti kutoka Wakala wa meli Tanzania (TASAC),Mhandisi Lameck Sondo alikiri kuwepo kwa malalmiko na ukiukwaji wa haki za mabaharia na kwamba tayari serikali kupitia Wizara ya uchukuzi na Mamlaka ya udhibiti na usafiri majini (TASAC) imeanza kulifuatilia jambo hilo kuhakikisha wamiliki wa meli na wadau wote wanaowasimamia mabaharia ambao wanakiuka mikatana yao wanachukuliwa hatua za kisheria.
Sondo alisema kuwa pamoja na hilo Shirika la kazi Ulimwenguni (ILO) imeweka mkabata wa kusimamia mabaharia wa mwaka 2022 ambao unawataka wamiliki wa meli na wadau wote wanaosimamia mabaharia wanautekeleza ili kuhakikisha mabaharia wanapata stahiki zao na kuondoa unyanyasaji wa aina yeyote unaofanywa kwa mabaharia.
Akizungumza katika ufunguzi huo Mkurugenzi wa mamlaka ya usafiri Zanzibar (ZMA), Mtumwa Saidi alisema kuwa wanajua uwepo wa changamoto za ukiukwaji wa mikataba kwa mahabaria na kwamba ZMA na TASAC wanasimamia kwa karibu kuona changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi sera,sheria za nchi na sheria za kimataifa.
Mwisho.



