UCHAMBUZI WA UDONGO KUONGOZA UZALISHAJI WA MBOLEA MPYA TANGA
Jun 23, 2026
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
KATIKA hatua inayotarajiwa kuongeza tija kwa wakulima nchini, Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imesema mbolea zitakazozalishwa katika kiwanda kipya kinachotarajiwa kujengwa mkoani Tanga zitakuwa zinatengenezwa baada ya kufanyika uchambuzi wa rutuba ya udongo wa maeneo husika.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TFC, Nuru Mhando, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo katika Wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea jijini Dodoma, amesema matumizi ya teknolojia ya uchunguzi wa udongo yatawezesha kubaini mahitaji halisi ya virutubisho kabla ya mbolea kutengenezwa.
Amesema mfumo huo utaondoa changamoto ya matumizi ya mbolea zisizoendana na mahitaji ya udongo, hali ambayo wakati mwingine husababisha mavuno kuwa chini ya matarajio licha ya wakulima kutumia pembejeo hizo.
“Tunakwenda kuzalisha mbolea zinazozingatia matokeo ya uchambuzi wa udongo. Hii itamwezesha mkulima kupata mbolea inayokidhi mahitaji ya eneo lake na kuongeza ufanisi wa uzalishaji,” amesema Mhando.
Amesema kiwanda hicho kitakachojengwa mkoani Tanga ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mbolea nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wake, uwekezaji huo pia utaimarisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kusaidia kupunguza gharama zinazotokana na uagizaji wa pembejeo hizo kutoka masoko ya kimataifa.
Mhando amesema TFC imeendelea kusambaza mbolea kwa wakulima kupitia utaratibu wa ruzuku wa Serikali unaolenga kuwafanya wakulima wengi zaidi kumudu gharama za pembejeo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
Aidha, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuhakikisha wanafaidika kikamilifu na uwekezaji wanaoufanya katika shughuli za kilimo.
Amesisitiza kuwa matumizi ya mbolea zinazozalishwa kulingana na mahitaji ya udongo yatakuwa hatua muhimu katika kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kukuza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.
