WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUMU WAKUTANA NA VIONGOZI BUNGENI DODOMA
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
WATOTO wenye usonji (Autism), Down Syndrome na mtindio wa ubongo (Cerebral Palsy) pamoja na wazazi wao wamekutana na viongozi mbalimbali katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, ambapo wamewasilisha changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.
Mkutano huo umefanyika katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.
Akizungumza katika tukio hilo, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Asma Mwinyi Foundation ambaye pia ni Mbunge wa Welezo, Unguja, Asma Ally Hassan Mwinyi, alisema lengo la ziara hiyo ni kutoa nafasi kwa watoto wenye mahitaji maalumu na wazazi wao kueleza moja kwa moja changamoto zao kwa watunga sera na wadau wa afya.
Alisema bado kuna changamoto za unyanyapaa katika jamii, gharama za matibabu na ukosefu wa uelewa kuhusu hali za watoto hao, hali inayokwamisha upatikanaji wa huduma stahiki.
Kwa upande wao, wazazi walieleza changamoto wanazokutana nazo ikiwemo mzigo wa gharama za matibabu na huduma za malezi, pamoja na changamoto za kijamii zinazowakabili watoto wao katika jamii.
Wakizungumza katika ziara hiyo, wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe walisema baadhi ya hali kama usonji na mtindio wa ubongo zinaweza kugundulika mapema na zinahitaji huduma za haraka za kitabibu ili kuboresha maendeleo ya mtoto.
Wataalamu hao waliwasihi wazazi kuwahi kuwapeleka watoto hospitalini wanapoona dalili za changamoto za maendeleo badala ya kuchelewa au kutumia tiba zisizo rasmi.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16, yakilenga kuhimiza ulinzi wa haki za watoto na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma sawa bila ubaguzi.





