WAZIRI WA ELIMU PROF MKENDA APONGEZA WANAFUNZI WA ST DOMINIC SAVIO WALIOFANYA ZIARA YA KIMASOMO BUNGENI
NA MATUKIO DAIMA MEDIA DODOMA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewapongeza wanafunzi na walimu wa Shule za St Dominic Savio zilizopo mkoani Iringa kwa jitihada zao za kuimarisha elimu kupitia ziara za kimasomo katika taasisi mbalimbali za serikali, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililopo jijini Dodoma.
Prof. Mkenda alitoa pongezi hizo alipokutana na wanafunzi hao wakati wa ziara yao ya kimasomo bungeni, ambapo walipata fursa ya kujifunza namna shughuli za kutunga sheria, kuisimamia Serikali na kuwakilisha wananchi zinavyotekelezwa na wabunge.
Alisema kuwa ziara za aina hiyo zina mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi uelewa mpana kuhusu masuala ya utawala, uongozi na mifumo ya kidemokrasia nchini.
Akizungumza na wanafunzi hao, Prof. Mkenda alisema Serikali inaendelea kuhimiza taasisi za elimu kuandaa programu mbalimbali zinazowawezesha wanafunzi kujifunza nje ya madarasa ili kupata maarifa ya vitendo yanayokamilisha yale wanayofundishwa darasani.
“Nawapongeza sana wanafunzi na walimu wa St Dominic Savio kwa kuandaa na kushiriki ziara hii muhimu.
Kupitia ziara kama hizi, wanafunzi wanapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kuelewa namna taasisi za umma zinavyofanya kazi. Hii ni hatua muhimu katika kuwajenga kuwa viongozi bora wa baadaye,” alisema Prof. Mkenda.
Aidha, Waziri huyo aliwataka wanafunzi kutumia vyema fursa ya elimu wanayoipata kwa kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kuzingatia maadili mema yatakayowawezesha kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao, wanafunzi wa St Dominic Savio walieleza kufurahishwa na ziara hiyo, wakisema imewapa uelewa mkubwa kuhusu shughuli za Bunge na namna maamuzi muhimu yanavyofanyika kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya nchi.
Walisema kuwa uzoefu walioupata utawasaidia katika masomo yao pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uongozi na maendeleo ya jamii.
Walimu walioambatana na wanafunzi hao walimshukuru Waziri Prof. Mkenda kwa kukutana nao na kutoa nasaha pamoja na motisha kwa wanafunzi.
Walisema shule hizo zimekuwa zikitoa kipaumbele kwa ziara za kimasomo kwa lengo la kuwapanua wanafunzi maarifa na kuwajengea uwezo wa kufikiri kwa kina kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Ziara ya wanafunzi hao bungeni ni sehemu ya mkakati wa shule za St Dominic Savio wa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu jumuishi inayowawezesha kuelewa kwa vitendo masuala ya uongozi, utawala bora na maendeleo ya taifa.
Hatua hiyo imeendelea kupongezwa na wadau wa elimu kwa kuwa inachangia kuandaa kizazi chenye maarifa, uzalendo na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Tanzania yenye maendeleo endelevu.



