VETA YAONESHA BIDHAA ZINAZOTENGENEZWA NA WANAFUNZI WAKATI WA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetumia maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kuonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wanafunzi wake, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kutambua mchango wa mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Rasilimali Watu wa VETA, Eliaika Manyanga, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, alisema bidhaa zinazooneshwa zimetengenezwa na wanafunzi kwa kushirikiana na walimu wao kupitia mafunzo ya vitendo yanayotolewa katika vyuo vya VETA.
Alisema bidhaa hizo zinajumuisha vifaa mbalimbali vya matumizi ya nyumbani na ofisini vinavyotumiwa na makundi tofauti ya jamii, huku vikionesha kiwango cha ujuzi na ubunifu unaopatikana kwa wahitimu wa taasisi hiyo.
Manyanga alisema VETA inaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu yanayolenga kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajirika, huku akibainisha kuwa udahili wa wanafunzi kwa muhula mpya utaanza mwezi Julai mwaka huu.
Aidha, alisema usajili wa wanafunzi unafanyika kupitia mfumo maalumu unaorahisisha waombaji kupata nafasi katika kozi mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni Tanzu ya Ujuzi ya VETA, Mhandisi Marco Kapinga, alisema kampuni hiyo imekuwa ikitumia ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo ya VETA kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya taasisi na sekta mbalimbali nchini.
Alisema hadi sasa kampuni hiyo imezalisha bidhaa 825 ambazo zimesambazwa katika taasisi za serikali na hoteli mbalimbali zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Kapinga aliongeza kuwa kampuni hiyo pia inalenga kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaoweza kutumika katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi, ikiwemo Canada.
