WAIBA MWANAFUNZI SHULENI, WATAKA MILIONI 20 .
Na Abdallah AMIRI, Igunga
MAMA mmoja, Paulina Paulo anadaiwa kuiba mtoto ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Bulunde, Kata ya Ibologero, wilayani Igunga mkoa wa Tabora kisha kuondoka naye kusikojulikana.
Hata hivyo, Baba wa mtoto huyo, Mwanzalima Magishi amesema, wamepokea ujumbe kupitia simu ya mke wake alitumiwa ujumbe wa simu unaomtaka atoe shilingi milioni 20 ili mtoto wake aweze kurejeshwa, vinginevyo hawatompata.
Mama wa mtoto huyo, Rehema Mnadi akiwa kituo cha Polisi, Ibologero alisema tukio hilo limetokea Juni Mosi,2026 aliporudi nyumbani akitokea shambani alikuta mwanae hajarudi kutoka shuleni.
Alifuatilia shuleni na hakumkuta mwanawe na ndipo aliamua kwenda kwa Mwalimu Mkuu msaidizi, Maombi Kalimanzila.
Mwalimu Kalimanzila alimweleza kuwa mama mmoja amefika shuleni hapo na kujitambulisha yeye ni shangazi wa Paulina na amekwenda kumchukua kwa ajili ya kwenda kumpiga picha ya kwenda kumfungulia akaunti benki ya NMB.
Hata hivyo alisema kabla ya mama huyo kuondoka shuleni hapo, alimvua sweta mtoto huyo na kumvalisha koti na kuondoka naye kusikojulikana hadi sasa.
“Baada ya kutoridhishwa na majibu ya mwalimu mkuu, alikwenda kituo cha polisi kidogo cha Ibologero na Ofisi ya mtendaji wa kata ya Ibologero.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Ibologero Mwita Wambura, Juliana Emmanuel na Jumanne Kingo kwa nyakati tofauti wamesema wamesikitishwa na kitendo hicho cha kuibiwa mwanafunzi shuleni na kusema kuwa kuna uzembe uliofanyika kwa Mwalimu huyo kwani alipaswa kumhoji mama huyo.
Mtendaji wa Kata ya Ibologero, Robarth Mwagara amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema wananchi kwa kushirikiana na ofisi ya kata pamoja na jeshi la polisi wanaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema hakuwa na taarifa hizo, na kuahidi kuzifuatilia baada ya kumaliza kikao.
