TOSCI YAIMARISHA MSAKO DHIDI YA WAUZAJI WA MBEGU FEKI
Jun 20, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima media Dodoma
TAASISI ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeendelea kuimarisha msako dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji wa mbegu feki kwa wakulima nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda uzalishaji wa mazao na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora zenye tija.
Kauli hiyo imetolewa na Mtafiti na Mkaguzi wa Mbegu kutoka TOSCI Makao Makuu, Neema Yohana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.
Neema amesema kuwa tatizo la mbegu feki lilikuwa kubwa miaka ya nyuma na liliwasababishia wakulima hasara kutokana na mavuno duni, lakini kwa sasa limepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya lebo maalum za ubora zinazotolewa na TOSCI.
“Changamoto ya mbegu feki ilikuwepo kwa kiwango kikubwa miaka ya nyuma, lakini tangu tuanze kutumia lebo za ubora, tatizo hilo limepungua sana.
Tunaendelea kuimarisha ukaguzi na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na kughushi au kuuza mbegu feki kwa wakulima,” amesema.
Amefafanua kuwa TOSCI inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya pembejeo za kilimo nchini kote ili kubaini na kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyoweza kuwaathiri wakulima.
Kwa mujibu wake, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanaonyesha kuwa hatua zinazochukuliwa na taasisi hiyo zimezaa matunda, huku visa vya mbegu feki vikipungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Aidha, amesema ushiriki wa TOSCI katika maonesho hayo unalenga kutoa elimu kwa wakulima, wafanyabiashara wa mbegu na wananchi kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu bora pamoja na namna ya kuzitambua.
“Tunatoa huduma mbalimbali kwa wakulima na wafanyabiashara wa mbegu. Tumeona bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu, hivyo tunatumia fursa hii kuwaelimisha wananchi namna ya kutambua mbegu bora na zisizo bora ili waweze kufanya maamuzi sahihi wanaponunua mbegu,” amesema.
Sambamba na hilo, amewahimiza wakulima na wananchi kuhakikisha wanajiridhisha kuhusu uhalali wa mbegu wanazonunua kwa kutumia mfumo wa uhakiki wa TOSCI uliowekwa kwenye lebo za ubora.
Amesema mnunuzi anatakiwa kukwangua sehemu maalum ya lebo ya TOSCI iliyopo kwenye kifurushi cha mbegu na kufuata maelekezo kwa kupiga namba 14852#, ambapo atapata taarifa zinazothibitisha kama mbegu hiyo ni halali au la.
“Mbegu bora zilizothibitishwa na TOSCI zina lebo maalum za ubora. Mkulima anapaswa kukwangua lebo hiyo na kufuata maelekezo kupitia namba 14852#.
Mwisho wa zoezi hilo atapata ujumbe kwenye simu yake utakaoonyesha uhalali wa mbegu husika. Akipata taarifa zisizo sahihi, basi ajue mbegu hiyo inaweza kuwa feki,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya mbegu feki utasaidia Serikali na wadau wa sekta ya kilimo kuendelea kulinda maslahi ya wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Mwisho

