MCC SALIM ASAS ASIFU UCHAPAKAZI WA RAIS DKT SAMIA
Na Matukio Daima Media ,Iringa
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa(MCC) Salim Asas, amepongeza kwa kiwango kikubwa utendaji kazi wa serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa imefanikiwa kuleta maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali muhimu kwa ustawi wa wananchi.
Asas alitoa pongezi hizo leo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa. Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi na kuongozwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi.
Akihutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi, Asas alisema kuwa serikali ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya dhati katika kusukuma mbele maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta za elimu, afya, miundombinu, maji na nishati. Alibainisha kuwa mafanikio hayo yanaonekana wazi katika maeneo mengi nchini ambapo huduma za kijamii zimeendelea kuboreshwa na kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
Alisema kuwa kazi kubwa inayofanywa na serikali iliyopo madarakani inapaswa kupongezwa na kila Mtanzania mwenye nia njema na maendeleo ya nchi.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali yao ili iweze kutekeleza kikamilifu mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
“Tunapaswa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo. Serikali yake imeendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema Asas.
Pamoja na kuzungumzia maendeleo, Asas aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano uliopo nchini, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo yoyote ya kijamii na kiuchumi.
Alieleza kuwa bila amani haiwezekani kutekeleza miradi ya maendeleo wala kuvutia uwekezaji unaochangia kukuza uchumi wa taifa.
Huku wananchi waliohudhuria mkutano huo walieleza kuridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kukuza uchumi, huku wakiahidi kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kudumisha amani nchini.





