SANGA: USHIRIKIANO WA CRDB NA BUNGE BONANZA WAENDELEA KUZAA MATUNDA
Na Hamida Ramadhan, Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amesema udhamini wa CRDB Bank kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya bonanza hilo na kuimarisha nafasi yake kama jukwaa la kuunganisha wadau mbalimbali kupitia michezo.
Akizungumza katika Bunge Grand Bonanza lililofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Sanga amesema ushirikiano huo umewezesha bonanza hilo kuendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuvutia ushiriki mkubwa kutoka kwa wabunge, watumishi wa Bunge na wadau wengine.
Amesema mafanikio ya tukio hilo yanatokana na mchango wa wadau mbalimbali, huku CRDB Bank ikiendelea kuwa mshirika muhimu katika kufanikisha malengo ya kuhamasisha afya, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa washiriki.
“Tunajivunia kuona Bunge Bonanza likiendelea kukua kila mwaka hii ni kutokana na ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wetu, hususan CRDB Bank ambayo imeendelea kuwa nasi kwa miaka mitano mfululizo,” amesema Sanga.
Ametoa shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, pamoja na menejimenti ya benki hiyo kwa kuendelea kuunga mkono shughuli zinazolenga kuimarisha ustawi wa jamii kupitia michezo.
Sanga amesema mbali na kutoa huduma za kifedha, CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia programu za maendeleo ya jamii, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa taasisi zinazotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Aidha, amepongeza juhudi za benki hiyo katika kupanua shughuli zake ndani na nje ya nchi, akieleza kuwa hatua hiyo inachochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi una mchango mkubwa katika kufanikisha shughuli za maendeleo na kuleta manufaa kwa wananchi.
