NBS NA TASAC KUANZISHA SENSA MPYA YA VYOMBO VYA MAJINI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALA imeanza hatua za kuandaa sensa ya kitaifa ya vyombo vya majini na shughuli za ujenzi wa meli kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa taarifa zitakazosaidia kupanga maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini nchini.
Hatua hiyo inakuja kufuatia ushirikiano ulioanzishwa kati ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wakala wa Usimamizi wa Meli Tanzania (TASAC), taasisi ambazo zitaongoza zoezi hilo katika Tanzania Bara.
Viongozi wa taasisi hizo wamesema upatikanaji wa takwimu sahihi utasaidia kubaini kwa undani hali ya sekta ya usafiri wa majini, ikiwemo idadi ya vyombo vinavyofanya kazi katika bahari, maziwa na mito pamoja na changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Akizungumzia maandalizi ya zoezi hilo, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema nchi inahitaji taarifa za uhakika ili kuweka mikakati madhubuti ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kwa tija zaidi.
Amesema sensa hiyo itafungua fursa mpya za uwekezaji kwa kuwapa wadau picha halisi ya mahitaji na uwezo uliopo katika sekta ya usafiri wa majini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohammed Salum, alisema uzoefu uliopatikana katika sensa iliyofanyika miaka iliyopita umeonyesha umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi katika usimamizi wa vyombo vya majini.
Amebainisha kuwa taarifa zilizokusanywa hapo awali zilichangia kuongeza ufanisi wa usimamizi wa sekta hiyo na kusaidia taasisi husika kupanga matumizi ya rasilimali kulingana na mahitaji halisi yaliyobainika.
Kwa mujibu wa TASAC, sensa inayotarajiwa kufanyika sasa itakuwa pana zaidi kwa kuwa itajumuisha vyombo vya aina mbalimbali pamoja na shughuli za ujenzi wa meli, jambo litakalowezesha kupatikana kwa taarifa kamili zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
"Matokeo ya zoezi hili yanatarajiwa kusaidia kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, kuboresha utoaji wa huduma, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wa uchumi wa bluu katika maendeleo ya taifa, " Amesema Mkurugenzi huyo
Wadau wa sekta hiyo wametakiwa kushiriki kikamilifu na kutoa taarifa sahihi ili kuhakikisha takwimu zitakazopatikana zinaakisi hali halisi na kuwa msingi wa maamuzi ya maendeleo kwa miaka ijayo.
Mwisho


