MTANDA AFUNGUA MKUTANO WA TAGCO MWANZA, AWATAKA WANAMAWASILIANO KUELEZA DIRA 2050 KWA USHAHIDI
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amewataka wanamawasiliano wa Serikali nchini kutumia taaluma yao kuifanya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iweze kueleweka kwa wananchi wa kawaida na isibaki kwenye maandiko.
Hayo ameyabainisha leo Juni 2, 2026 jijini Mwanza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka na Kongamano la Wanamawasiliano wa Serikali Tanzania (TAGCO) 2026, linalofanyika chini ya kaulimbiu “Taifa Moja, Sauti Moja Kuwasiliana Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Mtanda amesema kuwa mkutano huo unapaswa kuwa jukwaa la kubadilisha namna Serikali inavyowasiliana na wananchi ili Dira 2050 isibaki kuwa nyaraka za maandishi bali iwe sehemu ya uelewa wa wananchi wote.
Amesema kuwa mawasiliano ya sekta mbalimbali yanapaswa kuonesha namna yanavyochangia maendeleo ya taifa, na kuwataka wanamawasiliano kutumia takwimu sahihi, mifano halisi na ushahidi katika utoaji wa taarifa ili kuongeza uaminifu kwa wananchi.
“Tusiwasiliane kwa hisia pekee wala kauli za jumla, bali tuwasiliane kwa ushahidi. Wananchi wanahitaji kuona huduma zimewafikia watu wangapi au ni ajira zipi zimezalishwa kupitia miradi mbalimbali,” alisema Mtanda.
Mtanda alisisitiza kuwa wananchi hawahitaji kupokea takwimu nyingi zisizoeleweka, bali wanahitaji taarifa zinazoonesha namna utekelezaji wa sera na miradi unavyogusa maisha yao moja kwa moja.
Katika hatua nyingine,alifafanua kuwa Tanzania imeongeza juhudi za kujitangaza katika majukwaa ya kikanda na kimataifa kwa kueleza mafanikio yake kwa ubora na ushahidi, akibainisha kuwa nchi ina fursa nyingi za uwekezaji, utalii, madini pamoja na miradi ya kimkakati ambayo inahitaji kutangazwa zaidi
“Tanzania inahitaji simulizi moja yenye sura nyingi ikijumuisha maendeleo, uwekezaji, utalii, miundombinu, mazingira, utamaduni na amani,” Alisema Mtanda
Aidha, ameeleza kuwa dhana ya “Taifa Moja, Sauti Moja” haimaanishi taasisi zote kutumia maneno yanayofanana, bali kuwa na mwelekeo mmoja wa kitaifa unaounganishwa na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka maafisa habari kujenga simulizi sahihi kuhusu uwekezaji wa miundombinu ili wananchi waweze kunufaika na ajira pamoja na fursa zinazotokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mwenyekiti wa chama cha maafisa Mawasiliano wa serikali (TAGCO) Karimu Meshack ameleza kuwa Utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo 20250 inaweka msingi wa watanzania wenye uchumi wa kisasa wenye ushindani wa kimataifa unaotegemea maarifa, ubunifu kwa njia ya rasilimali watu na ujuzi wa hali ya juu.
Meshack ameeleza kuwa Katika kufanikisha maono hayo mawasilaino yanapaswa kuwa daraja kati ya sera na wananchi na wananchi wanahitaji kuelewa malengo ya taifa, ushiriki katika utekelezaji wake na kuona matokeo ya juhudi zinazofanywa na serikali katika maisha yao ya kila siku
Aidha ameleza kuwa mafaniko ya dira ya 2050 hayataamuliwa na ubora wa sera na miradi pekee bali kwa namna wanavyowasiliana na wananchi kuhusu dira ya maendeleo ya taifa 2025.
Mkutano huo wa TAGCO 2026 umezikutanisha wanamawasiliano wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini kujadili mikakati ya kuimarisha mawasiliano ya Serikali, kukuza taaluma, maadili na uratibu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





