Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 GRAND CHALLENGES TANZANIA KUFUNGUA MILANGO YA UBUNIFU, SULUHISHO ZA MAENDELEO

GRAND CHALLENGES TANZANIA KUFUNGUA MILANGO YA UBUNIFU, SULUHISHO ZA MAENDELEO

Na Hamida Ramadhan, Matukio,Daima Media Dodoma

SERIKALi imesema uzinduzi wa programu ya Grand Challenges Tanzania ni hatua muhimu katika kuimarisha utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia kwa lengo la kupata suluhisho endelevu za changamoto zinazoikabili Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika jijini Dodoma Juni 4, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, alisema mpango huo unatoa fursa ya kipekee kwa watafiti na wabunifu wa ndani kuendeleza mawazo yatakayochangia maendeleo ya taifa.

"Kupitia programu hii, sekta mbalimbali zitanufaika na matokeo ya tafiti na bunifu zitakazosaidia kuboresha huduma za afya, hususan afya ya mama na mtoto, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ustawi wa kijamii na kiuchumi, " Amesema.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu huku akihimiza ushiriki wa wadau kutoka sekta za umma na binafsi ili kuhakikisha matokeo ya programu hiyo yanawafikia wananchi na kuleta mabadiliko chanya.

Kwa upande wake, Profesa Ladislaus Mnyone amesema Grand Challenges Tanzania inalenga kuhamasisha matumizi ya tafiti katika kutatua changamoto za maendeleo na kuongeza mchango wa bunifu katika kukuza uchumi wa nchi.

Amesema kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kunahitaji uwekezaji mkubwa katika ubunifu wenye uwezo wa kuongezwa thamani na kuuzwa sokoni, jambo litakalosaidia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema programu hiyo itaimarisha ushirikiano kati ya watafiti, wabunifu, taasisi za umma na sekta binafsi katika kutafuta majawabu ya changamoto zinazowakabili wananchi kupitia sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais amesema programu hiyo itakuwa kichocheo cha upatikanaji wa teknolojia na uwekezaji unaohitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maendeleo, hususan katika sekta ya afya.

Mwakilishi wa Taasisi ya Afya Ifakara, Honorati Masanja, alisema Grand Challenges Tanzania itatoa fursa kwa vijana na makundi mengine ya jamii kushiriki katika ubunifu unaolenga kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.

Programu hiyo inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wadau wa maendeleo, watafiti na wabunifu katika kuibua suluhisho za kudumu kwa changamoto za taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi unaotegemea maarifa, utafiti na teknolojia.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3