Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 WAZIRI ULEGA: VIJANA WANA UWEZO MKUBWA WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO

WAZIRI ULEGA: VIJANA WANA UWEZO MKUBWA WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAENDELEO

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Wizara imeamua kuwapa nafasi vijana katika shughuli za ubunifu na maendeleo kwa sababu wana uwezo mkubwa wa kufikiri kwa kina na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa katika sekta ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo za shindano la ubunifu jijini Dodoma, Ulega amesema vijana wana fikra mpya, ubunifu wa kisasa na mtazamo tofauti unaoweza kusaidia Serikali kupata suluhisho bora na la haraka katika changamoto za maendeleo, hususan sekta ya miundombinu na usafiri mijini.

Amesema ushiriki wa vijana unalenga si tu kuibua mawazo mapya ya ubunifu, bali pia kuwajengea uwezo wa kiutendaji kwa kuwaunganisha na uhalisia wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Vijana wana uwezo mkubwa wa kufikiri na kutoa suluhisho tunataka wawahi kuingia katika mfumo wa utekelezaji ili baadaye wawe sehemu ya mafanikio ya taifa,” amesema Ulega.

Aidha, Waziri huyo amebainisha kuwa kupitia mashindano ya ubunifu, Serikali inawapa wanafunzi nafasi ya kuunganisha elimu ya darasani na uhalisia wa kazi, jambo linaloongeza uelewa na uwezo wa kutatua changamoto kwa vitendo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamati ya Shindano hilo, Dkt. Daniel Matondo wa EQRB, alisema jumla ya maandiko 561 yaliwasilishwa kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambapo baada ya mchakato wa tathmini, maandiko 186 pekee ndiyo yaliyokidhi vigezo na hatimaye 10 bora kuchaguliwa.

Amesema mchakato huo ulifanyika kwa uwazi na haki kupitia kamati yenye wajumbe 14, iliyohakikisha kila andiko linapitiwa kwa umakini kabla ya kufanya maamuzi ya washindi.

Dkt. Matondo ameeleza kuwa vyuo vilivyoongoza kwa ushiriki ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (MUST) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Aidha amesema mapendekezo ya washiriki yalijikita katika kuboresha mipango miji, matumizi ya teknolojia ya kisasa kama akili mnemba (AI), uboreshaji wa miundombinu ya barabara, na kuimarisha mifumo ya usafiri mijini ili kupunguza msongamano wa magari.

Ameongeza kuwa baadhi ya mapendekezo yalihusu kukamilisha mtandao wa mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa flyover, pamoja na kuanzishwa kwa mifumo bora ya usimamizi wa trafiki katika miji mikubwa.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3