WAZIRI NDEJEMBI AMKATAA MSIMAMIZI MRADI WA UMEME KIGOMA
• Ataka ukaguzi wa fedha za mradi zilizotumika
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Waziri wa Nishati Deogratius Ndejembi ameeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma unaotekelezwa na kampuni ya DONGFANG Electric International Corporationo (DEC) huku akitaka kuondolewa eneo la mradi kwa mhandisi mkazi wa kampuni hiyo anayesimamia mradi huo Duan Longhai.
Waziri wa nishati Deogratus Ndejembi akipata maelezo ya utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme katika bwawa la Malagarasi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma kutoka kwa Meneja wa mradi huo Saidi Kimbanga
Waziri Ndejembi alisema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi huo ambapo amesema kuwa haridhishwi na hatua ya utekelezaji wa mradi huo ulipofikia ukilinganisha na kiwango cha pesa ambacho tayari kampuni hiyo imepewa kama malipo ya awali dola milioni 20 huku kazi zilizotakiwa kufanyika zikiwa hazijafikia hata nusu ya utekelezaji wake.
Kutokana na hilo Waziri huyo wa nishati alisema kuwa pamoja na kutoa maagizo ya kuondolewa kwa Mhandisi Mkazi wa kampuni inayotekeleza mradi huo pia ametoa maagizo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kufanya ukaguzi wa kazi ambazo zimeshatekelezwa hadi sasa ukilinganisha na pesa ambayo imeshatumika akitoa wiki mbili kwa kazi hiyo kufanyika na taarifa kuwasilishwa kwake.
“Tulichogundua hii kampuni haina uwezo na ilipata kazi hii baada ya kuomba kazi hii kwa gharama za chini kuliko waombaji wengine, hivyo tutaongea na Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ili aongee na Balozi wa China tupate taarifa kazi ya uwezo wa kampuni hiyo na kazi ambazo wameshafanya ili tuone hatua za kuchukua,”Alisema Waziri Ndejembi.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Razalo Twange alisema kuwa kwa sasa mkandarasi huyo yupo nyuma ya utekelezaji wa mkataba wake kwa asilimia 20 akiwa hajafanya kazi muhimu zikiwemo za ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kilometa 27 kuelekea eneo la mradi, nyumba ya kuzalisha umeme (Power house) na nyumba za watumishi.
mradi wa kuzalisha umeme katika eneo lgamba mto Malagarasi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma
Alisema kuwa mradi huo wenye gharama ya Zaidi ya shilingi Bilioni 370 tayari Mkandarasi kampuni ya DongFang Electrical International Corporation imeshalipwa dola milioni 20 za marekani kwa kazi hizo ambazo zilipaswa kuwa zimekamilika lakini miezi tisa sasa kazi hizo bado hazijafika hata nusu na TANESCO imefanya jitihada mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo ikiwemo kukutana na mamlaka za juu za uongozi wa kampuni hiyo.




.jpg)