WAKUU WA TAASISI ZA KILIMO WAJENGEWA UWEZO WA UONGOZI MOROGORO
May 10, 2026
Matukio Daima,Morogoro
WAKUU wa vyuo vya mafunzo ya kilimo, mifugo na uvuvi wanaoshiriki mafunzo mkoani Morogoro wanasema wamepata maarifa mapya yatakayowasaidia kusimamia taasisi zao kwa ufanisi na kutatua migogoro kwa njia ya kitaalamu.
Mafunzo hayo yanayoandaliwa na Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) yanajikita katika mada za utawala bora, usimamizi wa rasilimali watu, ushirikishwaji wa watumishi na maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Dk. Kelvin Mwita, anasema viongozi bora ni wale wanaoweza kusikiliza pande zote na kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya taasisi.
“Uongozi wenye maono hujenga mazingira ya kazi yenye amani na tija,” anasema.
Kwa mujibu wa Meneja Miradi wa SAT, Kashindye Salum, mafunzo hayo yanawalenga viongozi 48 wa taasisi za mafunzo na utafiti katika sekta ya kilimo na mifugo.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Witness Bashaka, ambaye ni Mkuu wa chuo cha Kilimo Kilimanjaro anasema maarifa yaliyotolewa yataboresha namna viongozi wanavyoshughulikia changamoto zinazojitokeza katika taasisi zao.
Kaimu mkuu wa idara ya taaluma saidizi kutoka wakala wa mafunzo ya mifugo LITA Dkt. Bakari Ngecha amesema SAT pia wamewawezesha namna Bora ya kuandaa mitaala mipya mitatu ya kufundishia baada ya iliyokuwepo awali kuonekana imepitwa na wakati.
Dkt Ngecha anasema mafunzo hayo ya uongozi na usimamizi yataleta tija kubwa kwenye taasisi anayoiongoza kwa kuwa yataimarisha dhana ya utawala bora.
Moja ya changamoto kubwa inayorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi ni ukosefu wa wataalamu wenye weledi na ufanisi katika utatuzi wa migogoro ndani ya taasisi wanazosimamia na katika jamii inayowazunguka, hali inayochangia sintofahamu wakati wa utekelezaji wa majukumu.
Mwisho


