TRA TANGA YAWAPIGA MSASA WANAWAKE, YASISITIZA NIDHAMU YA KODI KUFIKIA DIRA YA 2050.
May 15, 2026
Na Amina Saidi,
Tanga.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Tanga imewatunuku elimu ya kodi na fursa za kibiashara wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali mkoani hapa, ikiwa ni mkakati wa kutanua uelewa wa mifumo na sheria za kodi nchini ili kuwajengea mazingira rafiki ya ukuaji wa uchumi.
Akizungumza katika Kongamano la Wanawake na Kodi, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Castrol John, amesema Mamlaka hiyo inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa kundi hilo sasa limekuwa mstari wa mbele katika uzalendo wa kulipa kodi.
“TRA inatambua mchango wa wanawake na kwa sasa mmekuwa kielelezo cha uwajibikaji Nawaomba mwendelee na moyo huu wa kuwa mstari wa mbele katika ulipaji kodi wa hiari ili kwa pamoja tushiriki kulijenga Taifa letu,” alisema Meneja John.
Kiongozi huyo alihimiza wanawake hao kudumisha nidhamu ya biashara na kodi, huku akiahidi kuwa milango ya TRA iko wazi wakati wowote kutoa msaada wa kitalamu na ushauri kwa mfanyabiashara yeyote anayekabiliwa na changamoto za kiutendaji.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Ismail Masoud, aliipongeza hatua hiyo na kuwataka watumishi wa TRA kuzidisha kasi ya kutoa elimu kwa walipa kodi ili kuondoa mianya ya sintofahamu inayowakabili wafanyabiashara wengi mkoani Tanga.
“Niwaombe TRA msiishie hapa, endeleeni kutoa elimu kwa wingi ili kukomesha mbinu za ‘janja janja’ za kukwepa kodi Tunataka tushirikiane kikamilifu kufanikisha Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 kwa kuwa na mfumo wa kodi wa uwazi na uaminifu,” alisisitiza Masoud.
Aidha, Masoud alitoa shukrani kwa wadau wa maendeleo, ikiwemo programu ya Good Financial Governance (GFG) na Shirika la GIZ la Ujerumani, kwa ushirikiano wao na TRA katika kuhakikisha elimu ya kodi inafika kwa wanawake na makundi maalum katika jamii.
Naye Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Wanawake (TWCC) mkoani Tanga Aziza Ramadhan, alisema kongamano hilo limefungua ukurasa mpya kwa wajasiriamali kwani limewapa ujasiri wa kuendesha biashara kwa kufuata taratibu rasmi bila hofu.
“Wanawake wengi walikuwa wakikosa taarifa sahihi, jambo lililosababisha wengi kushindwa kupanua biashara zao kutokana na hofu ya kodi au kutokujua wajibu wao kisheria. Leo tumepata mwanga wa jinsi ya kukua kisheria,” alisema Aziza.
Mjasiriamali na Katibu wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Mwajuma Saidi, alibainisha kuwa elimu hiyo imemsaidia kuelewa umuhimu wa kuwa na Namba ya Utambulisho wa mlipa Kodi (TIN) kama kigezo muhimu cha kurasimisha biashara.
Alimalizia kwa kusema kuwa elimu hiyo imewasaidia wanawake wengi kubaini kuwa kodi si mzigo wa kuogopesha, bali ni chombo muhimu cha kuimarisha biashara zao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi wa nchi.

