Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BAJETI YA MALIASILI NA UTALII 2026/27 KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA NA KUKUZA UCHUMI

BAJETI YA MALIASILI NA UTALII 2026/27 KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA NA KUKUZA UCHUMI


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt, Ashatu Kijaji, amewasilisha Bungeni mjini Dodoma bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 akieleza kuwa serikali imejipanga kuimarisha sekta ya utalii na uhifadhi kwa lengo la kuongeza ajira, mapato na maendeleo ya wananchi.

Akiwasilisha hotuba hiyo Mei 15, 2026,Bungeni  Waziri Kijaji alisema bajeti hiyo inalenga kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa huku ikiboresha maisha ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya hifadhi.

Amesema katika mwaka mpya wa fedha, Wizara itaendelea kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori, misitu, nyuki na malikale sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Serikali imepanga kuboresha miundombinu katika maeneo ya utalii ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano na huduma za kijamii ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo na kuvutia wawekezaji pamoja na watalii wengi zaidi.

Waziri Kijaji amesema Wizara pia itaongeza nguvu katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kwa kutumia matukio mbalimbali ya kimataifa ikiwemo AFCON 2027 pamoja na mikutano ya kimataifa itakayofanyika nchini.

"Idadi ya watalii imeongezeka kutoka milioni 5.3 mwaka 2024 hadi milioni 5.9 mwaka 2025 huku mapato ya sekta hiyo yakiongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 hadi dola bilioni 4.4.," Amesema Dkt, Kijaji


Ameeleza kuwa zaidi ya ajira milioni 2.7 zinategemea sekta ya utalii, hali inayodhihirisha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

"Katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, Waziri huyo alisema Serikali itaendelea kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo ndege nyuki (drones), uzio wa umeme na vifaa vya kufuatilia mienendo ya wanyamapori, " Amesema.

Pia amesema Wizara imeanzisha mfumo mpya wa PAIS utakaorahisisha ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi watakaopata madhara yatokanayo na wanyamapori ndani ya siku saba hadi 14.

Mwisho





 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3