SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA UCHUMI WA VIWANDA NA BIASHARA NCHINI
Na Samwel Mpogole - Mbeya.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza sekta ya viwanda na biashara nchini kwa lengo la kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo wakati akifunga rasmi maonesho ya Mbeya Expo 2026 yaliyofanyika Jijini Mbeya na kushirikisha wawekezaji, taasisi za serikali pamoja na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Londo amesema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kukuza mitaji kwa wananchi na kuimarisha sekta binafsi ili ndani ya kipindi cha miaka mitano Tanzania iwe na uchumi wenye ushindani na unaowanufaisha wananchi wa kada mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Taifa ya Biashara Mkoa wa Mbeya (TNCC), Erick Sichinga amesema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau wa sekta za umma na binafsi, hatua iliyosaidia kuongeza ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji pamoja na kubadilishana uzoefu kati ya wafanyabiashara.
Sichinga ameongeza kuwa maonesho hayo yamefungua fursa mpya za biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa huku yakichochea maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla.
Nao baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wamesema wamefanikiwa kupata wateja wapya, kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kujifunza mbinu mbalimbali za kuboresha biashara zao kupitia ushiriki wao katika Mbeya Expo 2026.



