Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SAFARI YA NEMC KUWA MAMLAKA IMEIVA

SAFARI YA NEMC KUWA MAMLAKA IMEIVA

 

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeridhia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka na muswada wake unatarajiwa kuwasilishwa bungeni wakati wowote.


Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa, wakati wa kikao kazi baina ya NEMC na wadau wenye viwanda.

Naibu Waziri alisema serikali kwa upande wake imeshakamilisha mchakato mzima wa kuifanya iwe mamlaka kamili kwa kufanya mashauriano na wadau mbalimbali na wataalamu washauri.

Alisema mchakato huo utawasilishwa bungeni na baada ya hapo wananchi watapewa nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu muundo  wa mamlaka hiyo na kutaka wananchi kujitokeza kutoa maoni wakati huo

“Niwatoe hofu wananchi na wadau kwamba kwa NEMC kuwa mamlaka haimaanishi kwamba itakuwa inafanyakazi kwa mabavu mabavu au kwamba itamwonea mtu, badala yake ndipo itafanyakazi zake kistaarabu zaidi kwa hiyo msiogope,” alisema

Aidha, aliitaka NEMC kuhakikisha wananchi watakapoitwa kwenda kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya muswada huo kujitokeza kwa wingi wakiwemo wadau muhimu wenye viwanda.

“Nawaomba sana NEMC kipindi hicho kitakapofika wananchi na wadau wa viwanda wapewe taarifa waje kutoa maoni yao ili tutakapotunga sheria hiyo iwe shirikishi kwa watu wote kusiwepo na malalamiko kwa wananchi wetu,” alisema.

Naibu Waziri alisema amefurahi kuona namna wenye viwanda walivyojitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo muhimu na akaitaka NEMC ihakikishe vikao kama hivyo vinafanyika mara kwa mara.

Naibu Waziri, alisema amefurahi kuona mjadala umekuwa na manufaa makubwa sana kwani wamezungumza kuhusu mambo mengi yakiwemo ya uzingatiaji wa sheria na vibali vya tathmini ya athari kwa mazingira EIA.


“Tumejadiliana kwa kina kuhusu uwepo wa mambo ya mipango ya ardhi na mwingiliano na jamii ambayo haihusiani na viwanda kwenye maeneo ya viwanda tumejifunza mengi na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inawapongeza kwa kushiriki mkutano huu na kutoa maoni yenu,” alisema


Alisema kwenye mkutano huo wamejadiliana kuhusu mifumo kusomana akitolea mfano kuwa wadau hao wameshauri  NEMC na Osha ziweze kusomana kwenye mifumo yake ili kuwapunguzia mzigo wenye viwanda.


“Nawapongeza sana NEMC kwa kuanda kikao hiki, tunanaelekea uchumi wa Dola trilioni moja sasa ili tufike huko vikao kama hivi ni muhimu sana si tu kwamba kwasababu tu tunaenda kwenye miaka 40 tuwe tunafanya vikao kama hivi kila baada ya muda flani,” alisema


Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Immaculate Semesi alisema amefurahi kuona wenye viwanda wamejitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo na kwamba ameyapokea na atafikisha maoni yao kunakohusika.


Alisema changamoto zilizotolewa na wenye viwanda zitafikishwa sehemu husika ili mwaka ujao wa fedha waweze kuanza wakiwa na utaratibu mzuri wa kutunza mazingira pamoja na viwanda.


“Nawashukuru sana mmetoa maoni ya kuboresha, NEMC ni mama na kazi ya mama ni kulea tumepewa kazi ya kuwalea watumiaji wa mazingira ili kuhakikisha wanapozalisha kuna kuwa hakuna uhalibifu wa mazingirana  wote tunapata manufaa makubwa,” alisema


“Mapenzi ya mama wakati mwingine ni kufinya kwaajili ya kurekebishana. Hatutaki kuwaumiza tunataka tufuate sheria na kanuni, sisi tunataka kufanya kazi ya kusimamia mazingira kidijitali ili tutoe huduma sahihi na kwa wakati na yenye   haki,” alisema


“Kwa sasa tuna mfumo wetu wa ukaguzi kidijitali unaitwa mazingira APP na mfumo wa zamani tunauboresha tunafanya kazi ya kuboresha mfumo wa tathmini athari kwa mazingira,” alisma

Alisema mwishoni mwa mwezi wa tano NEMC inaenda kuzindua mfumo wa ukaguzi wa kupima athari za viwango vya uchafuzi wa mazingira, hali ya hewa  na hali ya mitetemo.

“Mfumo huo wa kidijitali utapima kwenye APP yetu wote tutaona hakutakuwa na uonevu na mwisho wa  mwezi huu tutazindua mfumo unaoitwa Tanzania Online Continues Assessment Environment Emission System,” alisema 

Alisema mfumo huo umeshaanza kufanyakazi kwenye nchi za  Afrika kama Ghana, Nijeria na Kenya hivyo alisema wanataka mifumo yao iwe inasomana na kwamba unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia mwezi Julai

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3